Timu ya Madaktari Bingwa na Bobezi wa Mama Samia 42 walioweka kambi ya siku tano katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa) wamefanikiwa kuwatibu wagongwa 2,244 huku wagonjwa 74 wakifanyiwa upasuaji na wagonjwa 46 wakipatiwa rufaa ya kupata matibabu zaidi katika Hospitali ya Rufaa ya Bungando.
Akizungumza katika halfa ya kuhitimisha kambi hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya MK iliyopo Manispaa ya Musoma, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya amesema madaktari Bingwa madaktari hao wakiwa Mkoa wa Mara wamefanya kazi kubwa kwa manufaa ya maisha ya wananchi.
“Wananchi wa Mkoa wa Mara wanawashukuru sana na wangependa muendelee kutoa huduma hapa lakini wanafahamu huko mlipotoka pia wanawahitaji kwa ajili ya watu wengine kupata huduma” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amewakaribisha Madaktari Bingwa hao kama wanataka kuhamia au kuja kusaidia kutoa huduma za kibingwa katika hospitali hiyo au hospitali nyingine zilizopo katika Mkoa wa Mara na kuwaomba kama wanaushauri wa namna ya kuboresha huduma wautoe ili kuboresha utoaji wa huduma za afya katika Mkoa wa Mara.
Bwana Kusaya ambaye katika hafla hiyo alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi amewashukuru pia wataalamu wa afya wa Mkoa wa Mara walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika utoaji wa huduma katika kambi hiyo na kuwataka kuendelea kuwahudumia wananchi kwa weledi.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu amesema katika kambi hiyo, Hospitali ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere imefanikiwa kukusanya shilingi milioni 186 ambazo ni fedha taslimu na madai ya bima za afya zilizohusika katika kambi hiyo.
“Hospitali imetumia milioni 30 kwa ajili ya kulipa stahiki za watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere walioshiriki kwenye kambi hiyo pamoja na maandalizi ya kambi hiyo” amesema Dkt. Masatu
Dkt. Masatu amewashukuru viongozi wa Mkoa wa Mara, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Afya kwa kuandaa na kuratibu kambi maalum ya matibabu ambayo imesaidia katika kuwapatia matibabu ya kibingwa na bobezi wananchi wa Mkoa wa Mara.
Dkt. Masatu amezishukuru Hospitali zote za Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Hospitali za Rufaa za Kanda za Chato na Bugando kwa kuwaruhusu na kuwawezesha Madaktari Bingwa na Bobezi walioshiriki katika kambi hiyo maalum ya siku tano.
Akizungumza wakati wa kuwakaribisha viongozi katika hafla hiyo, Mganda Mfawidhi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Dkt. Osmund Dyegura amesema kambi maalum ya madaktari bingwa wa Mama Samia katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ilianza mwaka 2022 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu.
Dkt Dyegura amesema tayari Kambi kama hiyo mbali na Mkoa wa Simiyu pia imeshawahi kufanyika katika Mkoa wa Kagera na sasa Mkoa wa Mara na kote imekuwa ikileta manufaa makubwa kwa wananchi wanaopatiwa huduma.
Dkt. Dyegura amesema malengo ya kambi hiyo kusogeza huduma za kibingwa jirani na wananchi, kuwajengea uwezo wataalamu wa afya, kuibua wagonjwa ambao watapelekwa kupata matibabu zaidi katika Hospitali za Rufaa za Kanda.
Kambi ya Madaktari Bingwa na Bobezi wa Mama Samia imefanyika kuanzia tarehe 2-6 Desemba, 2024 na madaktari hao wakati wanawasili walipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi tarehe 2 Desemba, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa