Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo ameongoza mapokezi ya madaktari bingwa 45 katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuwataka wananchi kutumia vizuri fursa ya uwepo wa madaktari hao kupata matibabu.
Akizungumza katika mapokezi hayo, Mhe. Mtambi amemshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha madaktari hao kufanya kambi maalum katika Mkoa wa Mara na kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi jirani na makazi yao.
“Kambi ya madaktari bingwa imewezekana kuletwa katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya awamu ya Sita katika Sekta ya afya ikiwemo kujenga miundombinu na kununua vifaa tiba na dawa” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema awali huduma za madaktari bingwa na wabobezi zimekuwa zikitolewa Mwanza, Dodoma au Dar es Salaam na wananchi walikuwa wakitumia gharama kubwa kusafiri lakini sasa wamepata bahati huduma hii inapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Mhe. Mtambi amesema kwa mwaka huu, hii ni mara ya tatu Madaktari Bingwa wanaweka kambi maalum katika Mkoa wa Mara ambapo katika miezi ya Juni na Novemba, 2024 madaktari bingwa walifika na kutoa huduma katika Hospitali za Halmashauri na Vituo vya Afya vya Kasahunga na Ikizu katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Mhe. Mtambi amesema uwepo wa madaktari hao unawahakikishia madaktari bingwa hao huduma nzuri ya afya ambayo itaboresha uhai wao baada ya kupata matibabu ya kibingwa na kibobezi kutokana kwa madaktari hao.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka wananchi kuendelea kufika katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere hata baada ya muda wa kambi hiyo kuisha kwa kuwa hospitali hiyo pia inao madaktari bingwa ambao wataendelea kutoa huduma hata baada ya muda wa kambi hii maalum kuisha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka amewakaribisha madaktari hao katika Wilaya ya Musoma na kuwataka wananchi wa Musoma kujitokeza kwa wingi kupata huduma kwa madaktari hao.
Mhe. Chikoka amewataka wagonjwa waliojitokeza kwa siku ya leo kuwa mabalozi wazuri wa huduma watakazopata katika Hospitali hiyo na kuwahakikishia kuwa huduma za madaktari bingwa katika hospitali hiyo ni endelevu.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu amesema wataalamu wa Afya katika Mkoa wa Mara wamefurahia sana ujio wa madaktari bingwa hao ambao watasaidia kuwajengea uwezo watumishi na kubadilishana uzoefu wa kutibu wagonjwa.
Dkt. Masatu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Afya kwa kuandaa kambi ya madaktari bingwa maalum kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Mara kuweza kupata matibabu hospitalini hapo.
Dkt. Masatu amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba na dawa katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na hivyo ujio wa madaktari hao utaboresha huduma wanazozitoa kwa wananchi.
Akizungumza katika mapokezi hayo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Dkt. Osmund Dyegura amesema katika madaktari hao madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake ni watano, madaktari bingwa wa upasuaji wanne, madaktari bingwa wa watoto wanne, madaktari bingwa wa upasuaji wa mifupa watatu.
Dkt.Dyegura amesema madaktari bingwa wa pua, sikio na koo wawili, madaktari bingwa wa macho wawili, daktari bingwa wa mfumo wa mkojo mmoja, daktari bingwa wa ngozi mmoja, daktari bingwa wa usingizi mmoja, daktari bingwa wa kinywa na meno mmoja na daktari bingwa wa figo na inni.
Dkt. Dyegura amesema historia ya kambi za matibabu za madaktari bingwa katika Hospitali za Rufaa zilianza mwaka juzi ambapo ilifanyika katika Mkoa wa Simuyu na baadaye ikaendelea katika mikoa mingine na kwa sasa ipo Mkoa wa Mara.
Dkt. Dyegura amesema manufaa ya kambi hiyo ni kusogeza hudumaza kibingwa kwa wananchi, kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta ya afya katika utoaji wa huduma na kuibua wagonjwa ambao watatibiwa katika Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Baada ya mapokezi hayo, Mhe. Mtambi amefanya ukaguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuzungumza na wagonjwa waliokuja kwa ajili ya kupata huduma za kibingwa kwa madaktari hao na kusikiliza kero za wananchi.
Hafla ya mapokezi ya madaktari bingwa imehudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma, baadhi ya watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na wagonjwa waliofika kwa ajili ya kupata matibabu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa