Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo amefanya ziara na kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na kuitaka Halmashauri hiyo kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi.
Bwana Kusaya ametembelea na kukagua miradi ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mara, Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Shule ya Sekondari mpa inayojengwa katika eneo la Mayolo na kumtaka Mkurugenzi kukamilisha miradi hiyo.
“Hii miradi utekelezaji wake umechelewa na fedha za kukamilisha miradi hii mnazo, niwaombe tuipe kipaumbele ili iweze kukamilika kwa wakati” amesema Bwana Kusaya.
Akiwa Shule ya Wasichana ya Mara Bwana kusaya amepiga marufuku Halmashauri kutaka kulipa madeni ya wazabuni wa miradi ya awali kwa kutumia fedha mpya zilizoletwa kwa ajili ya kuongeza miundombinu katika shule hiyo inayoendelea kujengwa katika eneo la Bulamba.
Aidha, ameikumbushia Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuhusiana na umuhimu wa kuongeza eneo la shule hiyo mapema ili kuweza kujenga majengo zaidi kulingana na mpango wa shule hizo za Wasichana za Mikoa hapa nchini.
Akiwa katika jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Bwana kusaya amekagua ujenzi wa jengo unaotekelezwa na Suma JKT na ukuta wa eneo hilo unaojengwa na mafundi wa kawaida miradi yote ikiwa inatekelezwa kwa mfumo wa force account.
Akiwa katika shule ya Sekondari inayojengwa katika eneo la Myola, Bwana Kusaya amemuagiza Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda Bwana Salum Mtelela kufanya kikao na Meneja wa TANESCO, RUWASA na TARURA ili kupata ufumbuzi wa namna ya kupata huduma za maji, umeme na barabara katika shule hiyo mpya inayoendelea kujengwa.
Aidha, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bwana George Mbilinyi kuwalipa wananchi wa eneo hilo ambao ni wajumbe wa kamati mbalimbali zilizosaidia kusimamia ujenzi wa shule hiyo kwa mujibu wa taratibu za manunuzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mara Mwalimu Nyaeri Suzan Mwisawa amesema utekelezaji wa mradi wa fedha za awamu ya pili unaendelea taratibu kutokana na baadhi ya wazabuni walioshinda zabuni kugoma kupeleka vifaa wakidai malipo yao.
Mwalimu Mwisawa amesema katika awamu hii majengo yanayojengwa ni vyumba vinne vya madarasa, jengo la Tehama, makataba, mabweni manne ya wanafunzi na majengo matatu ya nyumbe za walimu moja ikiwa ni (two in one).
Akizungumza katika mradi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bwana George Mbilinyi amesema Halmashauri iliuza baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa awamu ya kwanza ya mradi huo na kufanikiwa kukamilisha bweni moja kati ya mabweni sita ambayo hayakukamilika katika mradi wa awali.
Aidha, Bwana Mbilinyi ameeleza kuwa Halmashauri imepanga kukamilisha mabweni matano yaliyobakia kutokana na fedha zilizoombwa kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kukamilisha majengo hayo.
Aidha, ameahidi kuendelea kumfuatilia mzabuni aliyegoma kupeleka vifaa hadi alipwe ili aweze kupeleka vifaa hivyo kama alivyoahidi walipozungumza naye mara ya mwisho ili mafundi waweze kukamilisha majengo hayo kwa wakati.
Akizungumzia mradi wa jengo la Halmashauri, Bwana Mbilinyi amesema mradi huo umechelewa kutokana na Suma JKT kukosa fedha za kuwalipa mafundi na amelazimika kuwakopesha shilingi milioni 15 ambazo watakatwa wakishawasilisha madai yao ili mradi uweze kukamilika.
Aidha, amesema Halmashauri imelazimika kutoa zabuni ya ujenzi wa ukuta na baadhi za kazi za nje ya jengo kwa mafundi wengine ili ujenzi huo uweze kukamilika kwa wakati.
Katika ziara hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, baadhi ya Maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkurugenzi na watumishi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa