Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo atafungua rasmi kongamano la maonesho ya madini yanayowakusanya pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya madini katika Mkoa wa Mara yatakayofanyika kwa siku nne katika Manispaa ya Musoma.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake, Mhe. Mtambi ametoa ratiba ya kongamano la maonesho ya mwaka 2025 ambapo litahusisha maonesho ya siku nne yatakayofanyika katika uwanja wa Mukendo, Kongamano la siku mbili katika ukumbi wa Mwembeni Complex na matembezi ya kupongeza mafanikio ya miaka minne ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tangu kuingia kwake madarakani, Dkt. Samia amefanya mambo makubwa sana katika Mkoa wa Mara kuwainua wachimbaji wadogo ikiwemo kupeleka umeme katika maeneo ya wachimbaji wadogo, kujenga masoko ya madini, kutoa bure maeneo ya uchimbaji madini kwa vijana, kuwajengea uwezo wa masuala ya sheria na kuwawezesha uboresha maisha yao” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema kauli mbiu ya maonesho hayo ni “Tuimarishe Uwekezaji katika Sekta ya Madini Mkoani Mara, Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Maendeleo ya Taifa” na kuongeza kuwa kongamano hilo linafanyika kwa lengo lakuhamasisha uwekezaji katika sekta ya madini na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi.
Mhe. Mtambi amesema kutakuwa na mafunzo ya kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo kuhusu uwekezaji katika sekta ya madini kuanzia tarehe 4-5 Juni, 2025 katika ukumbi wa Mwembeni Complex na maonesho ya teknolojia za uchimbaji, uchenjuaji, kemikali na vilipuzi na watoa huduma katika sekta ya madini.
Mhe. Mtambi amesema jumla ya watu 5,000 wanatarajiwa kushiriki katika kilele cha kongamano hilo na ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadau mbalimbali waliochangia kufanikisha kongamano hilo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa