Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo ameongoza kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na kuwataka watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara kuwa na mawazo ya ubunifu.
Akizungumza katika kikao hicho, Bwana Kusaya amewataka watumishi kuongeza ubunifu katika miradi inayotekelezwa na Sekretarieti ya Mkoa na vyanzo vya ukusanyaji wa mapato ya Serikali ili kuboresha huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Mara.
“Kwa sasa ukusanyaji wa mapato ya Serikali hauridhishi na kuna huduma muhimu ambazo katika Mkoa wa Mara hazipo, ambazo kama Mkoa tunatakiwa kuhakikisha kutokana na umuhimu wake huduma hizo zinakuwepo” amesema Bwana Kusaya.
Amezitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa supermarket kubwa katika Manispaa ya Musoma, kuboresha Ukumbi wa Uwekezaji ili kuweza kutumiwa na watu wengi zaidi na kutafuta wawekezaji waweze kuboresha kantini na klabu zinazomilikiwa na Sekretarieti ya Mkoa.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu, Kaimu Katibu Tawala Bwana Pius Sango Songoma amesema kuwa katika Kipindi cha Julai, 2024 hadi Novemba, 2024 watumishi 44 wamepandishwa vyeo na nane wamebadilishwa vyeo na kurekebishiwa mishahara kwa wakati.
Bwana Songoma amesema katika kipindi hicho watumishi watano hawakuweza kupandishwa vyeo kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutofikisha alama 60 za utendaji kazi kupitia mfumo wa PEPMIS na kuwasistiza watumishi wote kujaza taarifa zao kwenye mfumo huo.
Bwana Songoma amesema ofisi hiyo imeshughulikia mafao ya wastaafu wanne kupitia mfumo wa PSSSF Portal na kuwashauri watumishi kuingia katika mfumo huo na kufuatilia michango yao badala ya kusubiri wanapostaafu.
Aidha, Bwana Songoma amesema katika kipindi hicho Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara wamefanikiwa kupatiwa mikopo ya jumla ya shilingi milioni 350 kutoka Wizara ya Fedha (Hazina) ili kuboresha maisha yao.
Akitoa elimu kuhusu mgongano wa maslahi Bibi Witness Boniface Msonge Afisa Mwandamizi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Ziwa amesema katika suala la mgongano wa maadili sio lazima mtu awe amenufaika kiuchumi, wakati mwingine malengo yake mengine yanakuwa yamefikiwa.
Bibi Msonge amesema chanzo cha mgongano wa maslahi ni pamoja na asili ya mwanadamu ambayo ni ya kujipendelea wenyewe na watu wa karibu yake; jukumu ya kijamii yanayohitaji fedha; kulipa fadhili au kuwapendelea ndugu, jamaa na marafiki.
“Wananchi wengi wanaimani kubwa na Serikali na watumishi wa Serikali kuhusu kuwajibika kuwapa huduma bora kwa maslahi yao na Tanzania kwa ujumla” amesema Bibi Msonge na kuwataka wajumbe kutokuivunja imani hiyo ya wananchi.
Bibi Msonge amesema kuna aina tatu za mgongano wa maslahi ambazo ni mgongano halisi wa maslahi ambao unakuwa umetokea, aina ya pili ni hisia za uwepo wa mgongano wa maslahi kutokana na dalili au viashiria mbalimbali, na aina ya tatu ni uwezekano wa kutokea mgongano wa maslahi hapo baadaye.
Bibi Msonge amesema mambo ambayo yanasababisha mgongano wa maslahi ni pamoja na kupokea zawadi, kutumia muda wa ofisi kufanya shughuli binafsi, kufanya biashara kwenye ofisi ambazo mtumishi anaifanyia kazi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Idara na Vitengo, Makatibu Tawala wa Wilaya, wawakilishi wa wafanyakazi na wawakilishi vya vyama vya wafanyakazi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa