Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI leo tarehe 13 Machi, 2025 imefanyaziara Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere maarufu kama Kwangwa iliyopo Manispaa ya Musoma na kupongeza maendeleo ya ujenzi yaliyofikiwa katika hospitali hiyo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Hassan Selemani Mtenga amepongeza maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo iliyoanza kujengwa miaka ya 1976 hadi wakati huu ikiwa katika hatua za ukamilishaji.
“Katika Mwaka huu wa Fedha (2024/2025), Serikali imeleta zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa ajili ya shughuli za ukamilishaji wa jengo hili na kazi ya ukamilishaji inaendelea” amesema Mhe. Mtenga.
Mhe. Mtenga ameitaka hospitali hiyo kwa kutumia mapato ya ndani kuanza kujenga ukuta kuzunguka hospitali hiyo kwa awamu ili kuondoa mwingiliano wa shughuli za hospitali na wananchi wanaolizunguka eneo hilo.
Aidha, Mhe. Mtenga ameitaka Serikali ya Mkoa kuongeza nguvu katika usimamizi wa ujenzi katika hospitali hiyo ili uwekezaji uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita uzae matunda na wananchi waweze kupata huduma bora za matibabu katika hospitali hiyo.
Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Christina Christopher Mnzava ameipongeza Wizara ya Afya na Mkoa wa Mara kwa kusimamia ujenzi wa hospitali hiyo na kwa sasa maendeleo makubwa yanaonekana na kuitaka Wizara kuendelea kufuatilia kwa karibu na mradi huu.
“Tulikuja hapa miaka mitatu iliyopita, Hospitali ya Rufaa bado ilikuwa inatumia majengo ya zamani kule mjini, Kamati yetu ilishauri hospitali ihamie huku tunashukuru ilihamia na sasa ujenzi umeendelea vizuri na hospitali inatumika” amesema Mhe. Dkt. Mnzava.
Dkt. Mnzava amepongeza Mkoa wa Mara na Wizara ya Afya kwa kazi nzuri inayoendelea katika hospitali hiyo na kuwataka wakandarasi kukamilisha kazi zao kwa mujibu wa mikataba ili hospitali hiyo iweze kutumika vizuri.
Akizungumza wakati wa kuikaribisha Kamati hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi ameipongeza Serikali kwa kuleta fedha za ukamilishaji wa Hospitali hiyo ambayo amesema imewapunguzia adha wananchi wa Mkoa wa Mara katika upatikanaji wa matibabu.
“Kwa huduma za kibingwa kutolewa hapa Musoma, hosipitali hii imekuwa mkombozi wa wananchi wa Mara, imewapunguzia umbali wa kusafiri, gharama za matibabu, muda wa kwenda kufuata matibabu na kwa sasa wanapata huduma hizo ndani ya Mkoa” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema tayari Serikali imeleta fedha zote za ukamilishaji wa hospitali hiyo na jukumu lililobakia ni kwa viongozi na wataalamu kuwasimamia wakandarasi ili waweze kumaliza kazi ya ujenzi kwa wakati na huduma ziweze kutolewa kama ilivyopangwa.
Mhe. Mtambi amesema kwa sasa Hospitali hiyo imeanza kupokea wagonjwa kutoka nchi jirani na hususan maeneo yanayopakana na Mkoa wa Mara ambao wanakuja kwa ajili ya kupata huduma za kibingwa karibu na maeneo yao.
Mhe. Mtambi amewakaribisha wabunge hao katika Mkoa wa Mara na kuwataka wajumbe wa kamati hiyo kuonja nyama choma na kichuri kabla ya kuondoka.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya afya umeleta manufaa makubwa sana katika uimarishaji wa huduma za afya hapa nchini.
“Kwa hivi sasa sekta ya afya imetengewa shilingi trilioni 6.7 na matokeo ya utekelezaji wa bajeti hii yanaonekana, huduma zimeimarika na hivi sasa tunapokea wagonjwa wengi kutoka nchi jirani wanaofuata matibabu hapa nchini” amesema Dkt. Mollel.
Dkt. Mollel amesema kutokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali uliofanyika katika hivi sasa idadi ya wagonjwa kutoka Mkoa wa Mara kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando imepungua kutoka wagonjwa 6,400 hadi 900 tu ambao kwa mwaka 2024 walipata rufaa ya kwenda Bugando.
Kwa upande wake, Bwana Innocent Gerald, Mshauri Elekezi wa mradi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi amesema kwa sasa utekelezaji wa mradi wa ukamilishaji wa hospitali hiyo unaendelea vizuri na umefikia asilimia 65 na kwa mujibu wa mkataba wanatakiwa kukamilisha Septemba, 2025.
Bwana Gerald amesema kwa maendeleo ya mradi yanavyoelekea, mradi utakamilika kwa muda uliopangwa na kwa sasa wakandarasi wote walioshinda zabuni mbalimbali wapo katika eneo la mradi na wanaendelea na kazi.
Wengine walioshiriki katika ziara hiyo ni Katibu Tawala wa Mkoa Bwana Gerald Musabila Kusaya, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka, Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma,Maafisa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa