Kamati ya Kudumu ya Bajeti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo imefanya ziara katika Mkoa wa Mara na kuupongeza Mgodi wa Barrick North Mara kwa kufanikiwa kupunguza malalamiko ya wananchi na kuboresha mahusiano na wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa na wajumbe wa kamati hiyo waliokuwa wanachangia mada na kuuliza maswali katika majadiliano baada ya mgodi kuwasilisha taarifa yake kwa wajumbe wa kamati hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma Mjini Mhe. Vedastus Mathayo Manyinyi amesema awali mgodi huo ulikuwa na ugomvi wa mara kwa mara na wananchi wanaouzunguka mgodi huo na tuhuma za mgodi kuchafua mazingira na kusababisha maji kuchafuka, kuua samaki lakini kwa sasa hali imetualia.
“Yaani kwa sasa kinachosikika zaidi ni sifa nzuri ya mgodi na sio malalamiko ya wananchi na viongozi wao kama ilivyokuwa awali, ninawapongeza sana kwa hatua zote mlizochukua kuboresha mahusiano na wananchi” amesema Mhe. Manyinyi.
Mhe. Manyinyi ameushauri Mgodi huo kuwafuatilia wazabuni wanaotoa huduma katika mgodi huo kuhusu malipo ya wafanyabiashara wengine wanaofanyanao biashara ambayo amesema kuna malalamiko kuwa wanachelewa sana kuwalipa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ludewa Mhe. Joseph Zacharius Kamonga ameupongeza mgodi huo kwa kuwekeza katika kujenga na kuboresha mahusiano na wananchi wanaouzunguka mgodi na watanzania kwa ujumla.
“Kwa kweli mnafanya kazi nzuri sana katika kuboresha mahusiano na wananchi, viongozi na Watanzania kwa kushiriki katika masuala mbalimbali ya kitaifa” amesema Mhe. Kamonga.
Aidha, Mhe. Kamonga ameutaka mgodi huo kuwajengea uwezo watumishi wazawa ili waweze kunufaika na ujuzi huo na kupandishwa madaraja na kupewa nafasi za uongozi katika mgodi huo na baadaye kuacha kuwatumia wazungu kama wataalamu kutoka nje.
Mhe. Kamonga pia ameutaka mgodi huo kuwajengea uwezo na kuwapa fursa mbalimbali za kujifunza viongozi wa Mkoa wa Mara ili waweze kunufaika na mgodi huo na kuboresha utendaji na uongozi wao kwa manufaa ya wananchi wa Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Mhe. Stella Ikupa Alex ameupongeza mgodi huo kwa kuboresha mahusiano na kutoa fedha nyingi za CSR katika miradi muhimu ya kijamii katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kuutaka mgodi huo kuendelea na jambo hilo.
Aidha, Mhe. Stella Ikupa Alex ameuomba mgodi huo kuwapa watu wenye mahitaji maalum nafasi za ajira katika maeneo ambayo wanaweza kufanyakazi zao vizuri pamoja na changamoto walizonazo.
“Maeneo kama utawala, uhasibu, shughuli za ofisini watu wenye mahitaji maalum tunaweza kufanya na kwa niaba yao ninauomba mgodi kutupatia kipaumbele ili kuongeza idadi ya watu wenye mahitaji maalum walioajiriwa katika mgodi huu” amesema Mhe. Stella Ikupa Alex.
Kwa upande wake, Meneja wa Mgodi huo Bwana Apolinary Lyambiko amesema kwa sasa mgodi huo umeajiri watumishi 6,105 na kati ya waajiriwa wote watanzania kwa asilimia 96 huku watumishi wanaotoka katika Mkoa wa Mara wakiwa asilimia 23 ya watumishi wote.
Bwana Lyambiko amesema kwa sasa mgodi huo umeanza kufanya jitihada za maksudi kuongeza ajira za wanawake na watu wenye mahitaji maalum ambapo amesema kwa sasa wanawake ni asilimia 13 ya waajiriwa wote huku mgodi huo ukiwa na watu wenye mahitaji maalum wanne.
Bwana Lyambiko amesema mgodi huo umeboresha taratibu zake za manunuzi na kwa sasa kipaumbele zinapewa kampuni za ndani ya nchi na Mgodi huo umekuwa ukitoa pia mafunzo ya biashara kwa kampuni za kitanzania ili kuwajengea uwezo wa kufanya biashara zao na kufaidika na biashara hizo.
Meneja huyo amesema kwa sasa asilimia 83 ya wazabuni wote wanaotoa huduma na vifaa mbalimbali ni kampuni za kitanzania na hivyo kuendana na kanuni za uchimbaji madini hapa nchini zinazotaka wazawa kupewa nafasi zaidi katika ajira na zabuni mbalimbali.
“Kwa mwaka 2024 dola za kimarekani milioni 575 zilitumika kwa ajili ya zabuni mbalimbali zilizotolewa kwa makampuni ya Watanzania” amesema Bwana Lyambiko.
Bwana Lyambiko amesema Mgodi huo unafanya vizuri na kujishindia makombe na tuzo katika mashindano mbalimbali na unajitahidi kuweka mazingira salama kwa ajili ya watumishi na wawekezaji wanaofanya biashara na mgodi huo.
Ziara hiyo imeongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Josephat Sinkamba Kandege aliyeambatana na wabunge wengine na maafisa kutoka Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Bunge la Tanzania.
Ziara hiyo pia ilihudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Meja Edward Gowele, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa