Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 14 Mei, 2024 amefanya ziara katika Vijiji vya Mikomalilo Wilayani Bunda na Remung’orori Wilaya ya Serengeti kukagua athari za vurugu zilizotokea tarehe 12 Mei, 2024 na kuliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata wote waliohusika na vurugu hizo.
Mhe. Mtambi amefikia hatua hiyo baada ya kuvitembelea vijiji hivyo na kukagua athari za vurugu hizo ambapo watu tisa wamejeruhiwa na baadhi ya makazi ya muda ya wafugaji kuharibiwa katika vijiji hivyo kufuatia mgogoro wa ardhi ambao umekuwa ukiibuka na kufifia katika eneo hilo kuanzia mwaka 1954 hadi sasa.
“Ninaagiza watu wote waliohusika katika kufanya vurugu zilizotokea tarehe 12 Mei, 2024 wakamatwe mara moja na wafikishwe mahakamani” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi wa vijiji hivyo kuacha kukuza mambo kuhusiana na athari za vurugu zilizotokea tarehe 12 Mei, 2024 katika eneo hilo na kuwataka kuacha kujichukulia sheria mkononi jambo ambalo amesema linasababisha vurugu ndogo kuwa jambo kubwa bila sababu.
“Hamwezi kutatua tatizo kwa kutengeneza tatizo jingine kubwa zaidi kuliko tatizo la awali, Serikali haitamvumilia mtu yoyote anayejichukulia sheria mkononi na kusababisha vurugu katika eneo hili” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi amewataka wananchi kuendelea na shughuli zao za kawaida katika eneo hilo wakati Serikali inaangalia ufumbuzi wa kudumu kuhusiana na mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu katika vijiji hivyo.
Akiwa katika mkutano huo, Mhe. Mtambi amewaonya wananchi wanaopenda kuanzisha vurugu katika eneo hilo kuwa watachukuliwa hatua za kisheria na mashambuliano yote katika eneo hilo ametaka yakome kuanzia sasa na Wakuu wa Wilaya za Serengeti na Bunda wasimamie amani na utulivu katika eneo hilo.
Kanali Mtambi amesema hamna sababu ya kuendelea kuukuza mgogoro huo na hamna sababu ya wananchi wa vijiji hivyo kubaguana wenyewe kwa wenyewe na kuwataka wazee wa eneo hilo kulinda amani na utulivu wakati Serikali inaendelea kutafuta suluhisho la kudumu la mgogoro huo.
Amewataka wananchi wa vijiji hivyo kupitia viongozi wa vijiji kuwasilisha maoni yao kuhusiana na mgogoro huo kwa viongozi wa Wilaya ili maoni yao yawasilishwe mkoani ili yaweze kuangaliwa na wataalamu na watapata mrejesho.
Wakati huo huo, Kanali Mtambi ametaja sababu zinazochochea migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Mara linatokana na sehemu kubwa ya Mkoa wa Mara kuwa ni Ziwa Victoria asilimia 36 na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti asilimia 36 huku ardhi ya shughuli za kilimo, makazi, migodi, maofisi na viwanda ni asilimia 28 tu ya eneo la Mkoa wa Mara huku kukiwa na idadi kubwa ya watu.
Mhe. Mtambi ameitaja sababu nyingine ya migogoro ya ardhi ni kuwa wafugaji wa Mkoa wa Mara hawahami kutatufa malisho mikoa mingine na hivyo kuendelea kuongeza wafugaji na mifugo wakati eneo lililopo tayari ni dogo na hivyo kuchochea migogoro ya mara kwa mara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mikomalilo, Wilaya ya Bunda Bwana Joseph Wambura Machali ameeleza kuwa mgogoro katika eneo hilo ulikuwa umetualia hadi tarehe 12 Mei, 2024 ambapo vurugu ziliibuka katika eneo hilo.
Bwana Machali amesema chanzo cha vurugu hizo ni Bwana Magoto Magwaigu mkazi wa Kijiji cha Mikomalilo kwenda katika eneo hilo kufuata miti aliyokuwa ameikata tarehe 11 Mei, 2024 ndipo alipovamiwa na watu na akapiga yowe na watu wengine wakaja kumsaidia.
Bwana Machali ameeleza kuwa walipoona vurugu zinazidi kuongezeka wakapiga simu polisi ambao walifika wakati vurugu zikiwa zinaendelea na kusaidia kuzima vurugu hizo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mtambi ameambatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya za Bunda na Serengeti, baadhi ya maafisa kutoka Sektretarieti ya Mkoa, Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mara na maafisa kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa