Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya urithi wa dunia yaliyofanyika katika Uwanja wa Sokoine katika Mji wa Mugumu na kuwataka waandaaji wa maadhimisho hayo kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa umma kuhusiana na uhifadhi ya Maeneo ya Urithi wa Dunia.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Mtambi ameutaka Mkoa wa Mara na taasisi zinazohusika na maadhimisho hayo kuhakikishwa yanafanyika kwa ukubwa unaostahili kutokana na umuhimu wake katika uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Ninatamani kuona maadhimisho haya yakiwahusisha wananchi wengi zaidi na kutoa hamasa kubwa kwa wananchi wa Mji wa Mugumu na maeneo jirahi ili kuweza kuhifadhi Hifadhi ya Taifa ya Serengeti” amesema Mtambi.
Mhe. Mtambi ameagiza Mhe. Mtambi amewapongeza waandaaji wa maadhimisho hayo na kuagiza kuwa kwa mwaka ujao maadhimisho yahusishe mashindano ya insha na michezo mbalimbali na washindi wa mashindano haya wapewe tuzo katika kilele cha maadhimisho ya Maeneo ya Urithi wa Dunia yanayofanyika tarehe 05 Mei, 2025.
Kanali Mtambi amewataka washiriki wa kilele cha maadhimisho hayo kuwa mabalozi kwa kuwaelimisha wengine ambao hawajafika katika maadhimisho hayo ili kusambaza elimu iliyotolewa kwa wananchi na wadau wengi zaidi katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kutekeleza maagizo aliyoyatoa Mei, 2024 katika Kijiji cha Mbalibali yaliyolenga kutatua migogoro baina ya Hifadhi na wananchi na kupongeza kwa namna TANAPA ilivyotekeleza maagizo hayo na kumaliza kero za wananchi wa eneo hilo.
Mhe. Mtambi ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kwa upande wake, Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti SACC Stephano Msumi amesema Tanzania ina jumla ya vituo saba ambavyo vimefanikiwa kupata hadhi ya Maeneo ya Urithi wa Dunia vilivyopo katika maeneo mbalimbali.
“Afrika kuna maeneo ya Urithi wa Dunia 147 na kati ya hivyo, Tanzania ina maeneo saba ambayo yanahusisha maeneo ya hifadhi, mapori tengefu, misitu na maeneo ya kihistoria” amesema Mhe. Msumi.
Bwana Msumi amevitaja vituo hivyo kuwa ni pamoja na Hifadhi za Taifa za Serengeti na Kilimanjaro, michoro ya miambani Kondoa, Mji Mkongwe- Zanzibar, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Pori la Akiba Serous na magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeitangaza tarehe 05 Mei ya kila mwaka kuwa siku maalum kwa Bara la Afrika kusherehekea tunu ya urithi wa asili na kiutamaduni ya nchi wanachama.
Lengo la maadhimisho haya ni kuelimisha na kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa kutunza maeneo hayo pamoja na kutambua changamoto zinazoyakumba maeneo hayo ya urithi zitokanazo na migogoro, majanga ya asili, mabadiliko ya tabia nchi pamoja na shughuli za kibinadamu.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Majanga na Migogoro, Tishio la Maeneo ya Urithi wa Dunia” na kwa kiingereza ni Heritage Under Threat from Disaster and Conflicts.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wawakilishi kutoka Tume ya Taifa ya UNESCO, Ofisi ya UNESCO Tanzania, Wizara ya Maliasili na Utalii, mameneja wa vituo vyote vya Urithi wa Dunia kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar na Taasisi za Uhifadhi nchini.
Wengine waliohudhuria katika maadhimisho hayo ni pamoja na viongozi wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, wadau wa utalii, waandishi wa habari, baadhi ya wanafunzi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.