Wananchi wa Wilaya ya Musoma Mkoani Mara wameendelea kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, kwa kuondoa uhaba madawati mashuleni na kutengeneza kwa hiari yao na kuyakabidhi kwa Serikali madawati kadhaa ambapo Mei 6, 2025 zimepokelwa pea mia moja za meza na viti kutoka Jumuiya ya Waisilamu wa Manispaa ya Musoma.
Akipokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuliwekea msistizo suala la madawati kwa wanafunzi wa Mkoa wa Mara na hivyo kuwa suluhu ya changamoto ya madawati kwa wanafunzi.
“Mkuu wa Mkoa wa Mara amekuwa anasisitiza kuwepo mahusiano bora baina ya Serikali na taasisi zilizopo katika Mkoa zikiwamo taasisi za dini. Hongereni sana kwa kufanya jambo hili. Mkuu wa Mkoa amenielekeza nipokee madawati haya na anatoa asante sana” amesema Mhe. Chikoka.
Akizungumza katika hafla hii fupi mbele ya Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mara Shehe wa Mkoa wa Mara Ustadh Kassimu Msabaha amempongeza Mkuu wa Mkoa Mara kwa kushirikiana nao katika kila jambo analohusishwa.
Shehe Msabaha amesema Mhe. Mtambi anafanya mambo menngi mazuri ya kuileta jamii pamoja na kuongeza kuwa hilo ni jambo zuri na huo ndiyo utamaduni wa Watanzania.
Katika hafla hiyo risala ya makabidhiano iliyosomwa na Ustadhi Rashid Saad Kaema ilinadi kuwa “Sambamba na pea hizo 100 za meza na viti, Jumuiya ya Waisilamu Manispaa ya Musoma tutaendelea kushirikiana na Serikali zaidi na zaidi na kadili na majaliwa na Mwenyenzi Mungu.”
Akishukuru kwa Niaba ya Halmshauri ya Wilaya ya Musoma, Afisa Elimu Taaluma Bi Easter Kakulima amesema “tuna upungufu wa madawati 3548 na kwa msaada huu tuliopokea Jumuiya ya Waislamu wa Musoma wametuunga mkono na tunawashukuru sana, Mungu awabariki.”
Mara baada ya makabidhiano haya lilifanyika dua la kuiombea nchi ya Tanzania, kumuombea Rais Samia na kuuombea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na dua hii imeongozwa na Shehe wa Mkoa wa Mara Ustadh Kassimu Msabaha.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.