Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi leo ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Mara katika Wilaya ya Butiama na kuwataka watanzania kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo.
Akizungumza katika ziara ya miaka 61 ya Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar katika Wilaya ya Butiama, Dkt. Nchimbi amesema katika uhai wake Baba wa Taifa alihamasisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa na kukemea ubaguzi wa aina yoyote ile.
“Baba wa Taifa alipigania sana amani, umoja na mshikamano wa Tanzania na akaeneza lugha ya Kishwahili kwa Watanzania wote ili kuujenga umoja wa Kitaifa, tuendelee kumuenzi kwa vitendo kwa kuunga mkono mazuri yote aliyotuachia” amesema Mhe. Nchimbi.
Balozi Nchimbi amewataka Watanzania kujihadhari na viongozi wa siasa wanaohamasisha uvunjifu wa amani, ukabila na vurugu na badala yake kutumia uchaguzi unaokuja kuwachagua viongozi bora wanaopenda maendeleo.
Mhe. Nchimbi amesema miradi aliyoitembelea katika Mkoa wa Mara ya Uwanja wa Ndege Musoma, Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Chuo Kikuu cha MJNUAT Butiama ni miradi ya kimkakati na inaenzi maono na matamanio ya Mwalimu Nyerere na Serikali ya awamu ya sita imeitekeleza kwa ufanisi mkubwa.
Mhe. Nchimbi amewataka wanachama wa CCM na wananchi wa Wilaya ya Butiama kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kuhuisha taarifa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuhakikisha kuwa kura za CCM ni asilimia 100 ili kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amesema ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati katika Wilaya ya Butiama imebadilisha sura ya Butiama kimaendeleo.
Mhe. Sagini ameitaja miradi hiyo kuwa ni Chuo Kikuu cha MJNUAT Butiama, Sekondari ya Amali ya Mkoa wa Mara, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na Chuo cha VETA, mradi wa maji wa Mgango- Kiabakari- Butiama ambayo imelifanya eneo hilo kuwa eneo na hali tofauti kuliko lilivyokuwa awali.
Mhe. Sagini amemuomba Mhe. Nchimbi kuingiza mradi wa ukarabati wa Daraja la Kirumi lililopo katika Mto Mara katika Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2025-2030 ili daraja hilo liwekwe katika miradi ya kipaumbele katika utekelezaji wa ilani hiyo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Nchimbi ametembelea Kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ametembelea na kukagua ukarabati na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) Butiama na kuzungumza na wananchi katika Kampasi kuu ya chuo hicho na kuwasalimia wananchi katika eneo la Kiabakari.
Balozi Nchimbi ameambatana na viongozi na Watendaji wa CCM na Serikali na kauli mbiu ya miaka 61 ya Muungano ni “Muungano wetu ni Dhamana, heshima na tunu ya Taifa, Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.