Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 24 Aprili, 2025 ameshiriki ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi na kueleza kuwa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) Butiama ni sehemu za faida ya Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Akizungumza katika ziara ya miaka 61 ya Muungano Mhe. Mtambi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza maono ya Marais waliomtangulia kuhusu kujenga chuo kikuu kwa ajili ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Chuo hiki kilianza miaka ya 2010 lakini hadi Rais Samia anaingia madarakani (2021) kilikuwa hakijaanza kudahili wanachuo lakini Rais kutoka upande wa pili wa muungano ameleta fedha zilizowezesha wanafunzi kuanza kudahiliwa na ujenzi wa majengo mapya kuanza” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema Mhe. Samia ameweza kufanikisha ujenzi huu kutokana na msingi mzuri alioujenga Mwalimu Nyerere katika Taifa la Tanzania na kuongeza kuwa Rais Nyerere angekuwa mbinafsi Mkoa wa Mara ungekuwa na miradi mingi sana lakini miradi ya kimkakati inatekelezwa sasa na Rais kutoka Tanzania Zanzibar jambo ambalo bila ya kujengewa misingi mizuri lisingewezekana.
Mhe. Mtambi amesema MJNUAT ni mradi wa kipekee kwa kuwa hiki ni Chuo Kikuu cha umma cha kwanza kujengwa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na kinaenzi maisha na imani ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo.
Kanali Mtambi ameahidi Mkoa wa Mara kuendelea kusimamia ukamilishaji wa mradi wa ujenzi wa Kampasi Kuu ya Chuo hicho ili kukiwezesha Chuo kudahili wanafunzi wengi zaidi katika mwaka wa Masomo 2025/2026.
Mhe. Mtambi amesema katika ziara hii ya kuazimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanzania katika Mkoa wa Mara miradi mbalimbali ya kimkakati inatembelewa na kuzungumza na wananchi kuhusiana na faida za Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuuenzi na kuulinda Muungano wa Tanzania na kuwakemea wabaya wote wanaohatarisha Muungano kwa maneno na matendo yao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Prof. Caroline Nombo amesema Serikali ya Awamu ya Sita ilitoa fedha zaidi ya bilioni 2.6 kwa ajili ya kukarabati majengo ya iliyokuwa Sekondari ya Oswald Mwang’ombe na kuwezesha udahili wa wanafunzi kuanza.
Prof. Nombo amesema kwa sasa Chuo kina wanafunzi 78 wanaoendelea na masomo yao na kwa sasa kinayo mitaala na wataalamu na miundombinu ya kutosha kuwezesha kudahili wanafunzi wengi zaidi.
Prof. Nombo amesema Serikali kupitia mradi wa HEET umetoa fedha shilingi bilioni 102.5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Kampasi Kuu inayojengwa Butiama na majengo mengine katika Kampasi ya Tabora kwa ajili ya chuo hicho na ujenzi unaendelea vizuri.
Prof. Nombo amesema katika mipango ya baadaye Chuo hicho kinategemea kujenga Kampasi ya Tiba katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere katika eneo la Kwangwa.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara Mhe. Patrick Chandi Marwa amempongeza Rais kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea katika Mkoa wa Mara.
“Sisi kama Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara tunaridhika na utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 na tunaamini katika uchaguzi mkuu tutafanya vizuri kutokana na utekelezaji mzuri wa ilani” amesema Mhe. Marwa.
Mhe. Marwa amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi na viongozi na watendaji wote wa Serikali katika Mkoa wa Mara kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Nchimbi ameambatana na viongozi na Watendaji wa CCM na Serikali na kauli mbiu ya miaka 61 ya Muungano ni “Muungano wetu ni Dhamana, heshima na tunu ya Taifa, Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”.
Kesho ziara ya Katibu Mkuu wa CCM inaendelea ambapo atafanya mkutano wa hadhara katika Mji wa Shirati katika Wilaya ya Rorya, atatembelea mradi wa soko la kimkakati katika Mji wa Tarime na kuhitimisha kwa mkutano wa hadhara katika uwanja wa Serengeti katika Mji wa Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.