Adeladius Makwega-Musoma MARA.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi leo Agosti Mosi, amempokea na kuzungumza na Prof. Charles Lukiko Majige na kuzungumzaia umuhimu wa wananchi wa Mkoa wa Mara kulima zao la alizeti kutokana na kuwa na faida nyingi kwa wakulima.
“Natambua kuwa kilimo cha zao la alizeti kinatupatia mafuta ya kula, vyakula vya mifugo lakini pia kilimo cha alizeti kinasaidia kuzuia tembo kufanya uharibifu jirani na makazi ya binadamu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amempongeza Prof. Majige ambaye baada ya kustaafu ameamua kuwekeza kwa kujenga kiwanda cha mafuta ya alizeti na kulima katika eneo la Majita, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na kuwataka wananchi kuwaunga mkono wawekezaji wanaowekeza katika maeneo yao.
“Baadhi ya maeneo yetu, mtu akienda kuwekeza, madai yanakuwa huyu ni mtia, siyo kila anayewekeza ni mtia nia, watu wengi wanataka kuzikomboa jamii zao walipozaliwa sio kwa sababu za kisiasa” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi aamesema kuwa Mkoa wa Mara una wanyama pori wengi hususan katika maeneo yanayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na mapori ya akiba ya Ikorongo na Guremeti ambapo amesema tembo katika maeneo hayo wanaweza kudhibitiwa kwa kilimo cha Alizeti.
Mhe. Mtambi ameahidi Prof. Majige kuwa atashiriki kama mgeni rasmi katika tamasha la Kiutamaduni la kabila la Wajita litakalofanyika katika eneo la Bukima tarehe 15 Agosti, 2025 litakalohusisha ngoma, michezo, nyimbo na vyakula na matunda ya kiutamaduni wa kabila la Wajita.
Mhe. Mtambi amempongeza Prof. Majige kwa kuandaa tamasha hilo na kuongeza kuwa tamasha hilo ni uhimu katika kuifundisha jamii tamaduni na mambo mazuri yaliyokuwepo zamani ambayo kwa sasa yanapotea.
Aidha, Kanali Mtambi amemshukuru Prof. Majige kwa zawadi ya mafuta ya kula aliyompatia yaliyozalishwa katika kiwanda chake alichokianzisha.
Mhe. Mtambi amemuagiza Afisa Kilimo kutoka Sekretarieti ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kufuatilia upatikanaji wa mbegu za alizeti za ruzuku kwa wakulima kama sehemu ya kuwahamasisha kulima zao hilo ili kujiimarisha kiuchumi.
Kwa upande wake, Prof. Majige amesema amefungua kiwanda cha mafuta ya alizeti ili kuwahamasisha wananchi wa Mkoa wa Mara kulima alizeti kama zao la biashara na kuwaletea soko la uhakika la alizeti yao kupitia kiwanda hicho.
Prof. Majige amesema kuwa kiwanda hicho ambacho kipo katika eneo la Saragana kinauwezo mkubwa wa kuzalisha mafuta lakini kina changamoto ya kupata alizeti ya kutosha ili kiwanda hicho kiweze kufanyakazi kwa ufanisi.
Prof. Majige ambaye pia ni Chifu wa Wajita amesema kutokana na aina ya udongo uliopo, wananchi wakihamasishwa kulima kama zao la biashara, kilimo cha alizeti kinaweza kuwanyanyua kiuchumi kutokana na mahitaji ya alizeti katika viwanda vya ndani na nje ya Mkoa wa Mara.
Katika mazungumzo hayo Mkuu wa Mkoa alikuwa amewakaribisha maafisa mbalimbali kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.