Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza Serikali kutoa malipo ya asilimia 10 iliyobakia ya fidia ya wananchi wa mitaa minne ya Kata ya Nyatwali, Wilaya ya Bunda wanaohama kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Akizungumza wakati wa kuwasalimia Mji wa Bunda, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amemuagiza Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba kukamilisha malipo ya fidia ya asilimia 10 iliyobakia mapema iwezekanavyo.
“Nilizungumza na Mhe. Rais kuhusu malipo ya fidia ya Nyatwali na ameridhia fedha hizo zilipwe na mpaka sasa tayari asilimia 90 ya malipo ya fidia yameshalipwa imebakia asilimia 10 tu ya fidia hizo” amesema Mhe. Nchimbi.
Aidha, Balozi Nchimbi amewataka wananchi wenye malalamiko kuhusiana na fidia ya Nyatwali iliyotolewa kuyawasilisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara ili yaweze kushughulikiwa na Serikali.
Mhe. Nchimbi amewataka wananchi wa Bunda kutulia na kutoa malalamiko yao kwa ustaarabu wakati Serikali inaendelea kukamilisha malipo ya fidia hiyo na kuwahakikishia kuwa kwa namna anavyomfahamu Waziri wa Fedha fidia hiyo italipwa hivi karibuni.
Wakati huo huo, Mhe. Nchimbi amewataka wananchi kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu na kuacha kuwasikiliza viongozi wanaohubiri uvunjifu wa amani na vurugu katika uchaguzi huo.
“Awamu ya pili ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura karibu utafika kwa awamu ya pili, kwa wale wote wanaohitaji kuboresha taarifa tutumie fursa hiyo kuboresha taarifa ili kuweza kushiriki uchaguzi” amesema Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi amesema kutokana na uchaguzi mkuu kumekuwepo na vichocheo vya vurugu, uhasama na matukio ya uvunjifu wa amani na kuwataka wananchi wasikubali kuharibu amani iliyopo ambayo imedumu kwa muda mrefu na kujihadhari na matukio hayo kwani kuna maisha baada ya uchaguzi
Mhe. Nchimbi ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kukipigia kura Chama cha Mapinduzi kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM yam waka 2020-2025 hapa nchini.
Mhe. Nchimbi leo ameanza ziara ya siku tano katika Mkoa wa Mara ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar wenye kauli mbiu “Muungano wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa, Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”.
Mapokezi hayo yamehudhuriwa na viongozi wa CCM Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Bunda, watendaji wa umma, wanachama wa CCM na wananchi wa Wilaya ya Bunda na maeneo jirani.
Kesho ziara inaendelea katika Wilaya ya Musoma ambapo atakagua maendeleo ya ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma, kukagua maendeleo ya ujenzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, atatembelea Ofisi za CCM Mkoa wa Mara kukagua ukumbi wa mikutano wa CCM na kufanya kikao cha ndani na Halmashauri Kuu iliyoboreshwa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.