Mkuu wa mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amefungua Mkutano wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Mkoa wa Mara na kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuunga mkono shughuli za wanawake hapa nchini.
Mhe. Mtambi ameeleza hayo leo Februari 14, 2025 katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara wakati akizungumza na wanawake takriban 200 wanachama wa Chemba ya Wanawake Tanzania.
“Serikali inazo fursa nyingi kwa ajili ya wanawake ikiwemo mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa hapa nchini kwa ajili ya makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu” amesema Mhe Mtambi.
Mhe. Mtambi pia amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ikiwemo sera, sheria, kanuni na taratibu zinazowawezesha wanawake kufanya shughuli zao na hususan shughuli za uzalishaji mali bila kubaguliwa.
Mhe. Mtambi ametumia fursa hiyo pia kuwakumbusha wanawake wa Mkoa wa Mara kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika Mkoa wa Mara ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii na uchimbaji wa madini.
Wakati huo huo, Mhe. Mtambi amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kuhakikisha kuwa katika maonesho ya Kitaifa na Kimataifa wanawake wa Mkoa wa Mara wanapata nafasi na wanashiriki.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka wanawake wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ikiwa ni pamoja na kuwania nafasi mbalimbali zinazogombaniwa na kupiga kura ili kumchagua Rais, wabunge na madiwani.
Awali, akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa, Katibu wa Chemba ya wanawake Mkoa wa Mara Bi Anastazia Kirati amesema wanawake wajasiriamali wanapata changamoto katika kupata mikopo kutoka Serikalini na taasisi za kifedha.
“Wanawake wanapata changamoto ya kupata mikopo ambapo wapo wanaopata lakini hawana fursa ya elimu ya kutosha na hivyo kuwafanya kushindwa kuitumia vizuri mikopo hiyo.” Amesema Bi. Anastazia.
Bi. Anastazia ameiomba Serikali na taasisi za kifedha kutoa elimu ya biashara kwa wajasiriamali wanaopewa mikopo ili waweze kufaidika zaidi na mikopo hiyo kwa kuendeleza biashara zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kanda wa TWCC Bi Happines Mabula amesema kuwa chemba yao ilianzishwa mwaka 2005 sasa inakaribia kuwa na miaka 20 ikitoa huduma zake kwa wananwake wafanyabiashara na wajasiriamali hapa nchini.
Ufunguzi wa mkutano huo umehudhuriwa pia na baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.