7Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) imetiliana saini na Kampuni ya Saba Engineering kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Serengeti katika Halmashauri ya Serengeti, Mkoa wa Mara tarehe 27 Februari, 2025.
Akizungumza katika hafla ya kutia saini mkataba huo, Mkurugenzi Mkuu wa TAA Bwana Abdul Mambokaleo amesema Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uwanja huo katika mwaka wa fedha 2024/2025.
“Kampuni ya Saba Engneering imepewa mkataba wa miezi sita na baada ya kukamilisha upembuzi yakinifu itatoa ushauri wa kitaalamu wa namna bora ya kujenga uwanja huo” amesema Bwana Mambokaleo.
Bwana Mambokaleo amesema kuwa Serikali inajenga uwanja huo ili kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) pamoja na kurahisisha usafiri wa wananchi na mizigo kuingia katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Dkt. Maulid Suleiman Madeni ameipongeza TAA kwa kuchukua hatua za kutenga fedha na kuanza ujenzi wa uwanja huo na kusema kuwa uwanja huo utaleta mapinduzi ya kiuchumi kwa wananchi wa Serengeti.
“Baada ya uwanja huu kukamilika huu kukamilika watalii wote watashuka moja kwa moja Serengeti na kuingia hifadhini na wakati wa msimu wa utalii tunategemea kupata ndege hadi 100 kwa siku moja” amesema Dkt. Madeni.
Dkt. Madeni amesema uwanja huo utasaidia kuboresha uchumi wa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Mkoa wa Mara kwa ujumla kutokana na kujengwa kwa ofisi mbalimbali katika Mji wa Serengeti kama sehemu ya uwepo wa uwanja huo.
Dkt. Madeni amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanza kutenga fedha za ujenzi wa uwanja huo.
Uwanja huu unaongeza viwanja vya ndege vya Mkoa wa Mara kuwa viwili baada ya Serikali kutoa bilioni 35 kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege Musoma ambao pia unatarajiwa kusaidia kurahisisha usafiri kwa watalii wanaoingia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kutumia lango kuu la Ndabaka lililopo Wilaya ya Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.