Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo tarehe 11 Aprili, 2025 ametembelea ujenzi wa Shule ya Sekondari Kibumaye inayojengwa katika eneo la Mogabiri, Halmashauri ya Mji wa Tarime na kuagiza ujenzi wa shule hiyo ukamilike katikati ya mwezi Mei, 2025.
Akizungumza katika mradi huo, Mhe. Mtambi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kuhakikisha kazi ya ujenzi inafanyika usiku na mchana na inakamilika ili kuiwezesha shule hiyo kuanza kuchukua wanafunzi.
“Mimi nitapita kukagua utekelezaji wa mradi huu katikati ya Mei, 2025 nikute umekamilika la sivyo nikute hatua zimechukuliwa kwa yoyote aliyehusika katika kuukwamisha mradi huu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Meja Edward Gowele kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi huo na kumpa taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo mara kwa mara.
Akiwa katika eneo hilo Mhe. Mtambi ametembelea Shule ya Msingi Mogabiri na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kukarabati ofisi ya walimu wa shule hiyo na kutoa muda wa kuanzia leo hadi katikati ya Mei, 2025 ukarabati uwe umekamilika.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kufuatilia na kutoa taarifa ndani ya siku 14 kuhusu zabuni zote alizopewa Mzabuni aliyefahamika kwa jina la Mama Leah katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mara ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kuwa mzabuni huyo amepewa zabuni nyingi za kusambaza vifaa kwenye miradi inayotekelezwa katika Halmashauri nyingi za Mkoa wa Mara lakini hamna sehemu amefanya vizuri baada ya kushinda zabuni hizo kupitia kwenye mfumo wa NEST.
Akiwa katika Sekondari ya Julius Kambarage Nyerere, Mhe. Mtambi ameagiza mzabuni huyo asipewe zabuni nyingine mpya katika Mkoa wa Mara mpaka hapo atakapokamilisha utekelezaji wa zabuni alizonazo kwa sasa.
Mhe. Mtambi ametoa kauli hiyo baada ya kupokea taarifa kuwa mzabuni huyo amechelewesha pia utekelezaji wa mradi katika shule hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele amesema Mama Leah ameshinda zabuni katika miradi mingi inayotekelezwa katika Halmashauri za Wilaya ya Tarime na Mkoa wa Mara kwa ujumla na hana uwezo wa kusambaza vifaa hivyo kwa wakati.
“Kila alipopewa zabuni analalamikiwa kuwa hatekelezi kwa wakati na ameshinda zabuni nyingi katika miradi ya Serikali inayotekelezwa na Halmashauri za Mkoa wa Mara” amesema Mhe. Gowele.
Kwa upande wake, Diwani wa eneo hilo Mhe. Daudi Mrimi Wangwe amesema mradi huo unachelewa kutokana na mzabuni wa vifaa kuwakwamisha mafundi ambapo mara kwa mara vifaa kama vile matofali, mawe, mchanga, nondo na kadhalika anachelewa kuleta na hivyo kukwamisha kazi.
“Haya majengo yapo tayari muda mrefu lakini yeye pia anachelewesha kuleta mbao za kupaulia na kila wakati anatoa ahadi ambazo hazitekelezi kama anavyoahidi” amesema Mhe. Wangwe.
Mhe. Wangwe amesema Kamati ya Ujenzi wa mradi huo inapomfuatilia mzabuni huyo anatoa majibu ya kejeli kwa kamati hiyo na kuwapa ahadi za uongo mara kwa mara.
Awali, akitoa taarifa za ujenzi wa Shule ya Sekondari mpya ya Kibumaye, Mkuu wa Sekondari ya Mogabiri Mwalimu Magudila Mgeta amesema Shule ya Sekondari Mogabiri ilipokea shilingi 584,280,09/= tarehe 23 Juni, 2024 kutoka mradi wa SEQUIP na ujenzi wa shule hiyo umeanza Novemba, 2024 baada ya mchakato wa kupata vifungu na manunuzi kukamilika.
Mwalimu Mgeta amesema mradi kwa sasa upo asilimia 40 ambapo madarasa nane na maabara mbili zipo katika hatua za kupauliwa, maktaba ipo hatua ya boma, maabara moja na jengo la utawala yapo hatua za msingi wakati jengo la TEHAMA lipo katika hatua ya boma.
Mwalimu Mgeta amesema mradi umechelewa kuanza utekelezaji kutokana na fedha kuingia katika mwisho wa mwaka wa fedha wa 2023/2024, kukosekana kwa vifungu na tatizo la wazabuni kushindania zabuni na kukataa kazi na fedha iliyotumika ni shilingi 74,705,260 kwa ajili ya kulipia vifaa na mafundi.
Amesema kwa sasa wanasubiria mzabuni alete mbao za kuezekea na fundi mmoja aliyepewa kazi amepata ajali wanasubiria apate nafuu aendelee na kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sekondari ya Julius Kambarage Nyerere Mwalimu Melania Julius Gerald amesema Shule hiyo ilianza mwaka 2014 ikiwa na kidato cha kwanza hadi cha nne mchanganyiko na mwaka 2020 ilianza kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano wasichana.
Amesema kwa sasa Shule hiyo inawanafunzi 1056 na ina jumla ya walimu 24 na kwa sasa shule hiyo inatekeleza miradi mitano yenye thamani ya shilingi 216,400,000/= na kwa sasa ipo katika hatua mbalimbali.
Taarifa zote mbili za miradi hiyo zilionyesha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umechelewa kutokana na ucheleweshwaji wa vifaa kutoka kwa mzabuni aliyefahamika kama Mama Leah aliyeshinda zabuni ya usambazaji wa vifaa katika miradi hiyo.
Katika ziara hiyo Mhe. Mtambi aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, baadhi ya Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na wazabuni na mafundi wanaotekeleza mradi huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.