Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi leo tarehe 23 Aprili, 2025 ametembelea na kukagua Uwanja wa Ndege Musoma na ujenzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa) na kutoa wiki mbili kwa Wizara ya Fedha kuilipa TEMESA madai yake ili kutatua changamoto ya umeme katika Hospitali ya Kwangwa.
Mhe. Nchimbi ametoa maagizo hayo baada ya kupokea taarifa kuhusiana na madai ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ambao umepata zabuni ya kutengeneza mfumo wa umeme na jenerata kwa ajili ya Hospitali hiyo hajalipwa kwa muda mrefu na kukwamisha utoaji wa huduma katika hospitali hiyo.
“Ninamwagiza Waziri wa Fedha alipe deni hilo ndani ya wiki mbili ili TEMESA wakamilishe kazi yao na umeme wa kutosha uweze kupatikana katika hospitali hii. Baada ya wiki mbili nitakupigia simu Mkuu wa Mkoa kujua kama fedha hizo zimeshaingia” amesema
Mhe. Nchimbi ameahidi kuendelea kufuatilia utekelezaji na ukamilishaji wa miradi ya kimkakati katika Mkoa wa Mara na kuipongeza Wizara ya Afya na Mkoa wa Mara kwa utekelezaji wa mradi wa hospitali hiyo na usimamizi mzuri katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Dkt. Nchimbi ameipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kwa upanuzi wa uwanja huo wenye historia kubwa katika maendeleo ya Tanzania na kuitaka Wizara ya Fedha kulipa shilingi bilioni 2.5 anazodai mkandarasi wa uwanja huo ili uanze kutumika kuanzia Septemba, 2025.
Mhe. Nchi ameitaka TAA na Wizara ya Fedha kuona namna mchakato wa ujenzi wa jengo la abiria utakavyoweza kuharakishwa ili kupata jengo la kisasa la abiria katika Uwanja wa Ndege Musoma.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel amesema baada ya hospitali hiyo kuanza kufanya kazi imepunguza asilimia 70 ya rufaa kutoka Mkoa wa Mara kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jambo ambalo limesaidia kuokoa maisha ya wananchi.
Mhe. Mollel amesema Hospitali hiyo tangu imeanza kufanya kazi inatoa huduma nzuri kwa wagonjwa na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya Mkoa wa Mara kwa matibabu ya kibingwa kwa kuwa sasa yanapatikana Musoma.
Dkt. Mollel amesema Wizara ya Afya inalifanyia kazi ombi la kutoa eneo la Hospitali hiyo kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Tiba ili kuimarisha zaidi huduma za afya katika Mkoa wa Mara.
Awali, akitoa taarifa za mradi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Osmund Dyegula amesema Hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wengi kutoka nchi jirani na kwa mwaka huu pekee imehudumia wagonjwa 161 kutoka nchi za Kenya na Uganda.
Dkt. Dyegula amesema changamoto ya umeme ikitatuliwa itaiwezesha Hospitali hiyo kuhudumia wagonjwa wengi zaidi kutoka Mkoa wa Mara, Simiyu na nchi jirani na hususan wanaosumbuliwa na matatizo ya figo na waliopata ajali.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa uwanja wa ndege, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara Mhandisi Vedastus Maribe amesema uwanja huo utakapokamilika utawezesha ndege kubwa za abiria kuweza kutua na kuruka.
Mhandisi Maribe amesema tayari serikali imeshalipa fidia kwa awamu mbili jumla ya bilioni nane na wananchi 144 wamelipwa na kwa awamu ya tatu inahusisha wananchi 58 na gharama ya shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya eneo la kujenga jengo la abiria.
Mhandisi Maribe amesema ujenzi wa uwanja huo umetoa ajira kwa wataalamu mbalimbali 116 na kati yao wazawa 113 huku kukiwa na wataalamu watatu kutoka nje ya nchi.
Mhandisi Maribe anasema uwanja huo umechelewa kukamilika kutokana na ucheleweshwaji ya malipo ya mkandarasi lakini kwa sasa upo katika hatua nzuri.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mbunge wa Musoma Mjini Mhe. Vedastus Mathayo amesema Hospitali hiyo inachangamoto kubwa ya umeme jambo ambalo linazuia kutumia vifaa mbalimbali vilivyonunuliwa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa.
Mhe. Mathayo amemuomba Mhe. Nchimbi kufuatilia madai ya shilingi bilioni 1.5 yaliyowasilishwa na TEMESA tangu Desemba, 2025 ambayo hadi sasa hazijalipwa na mradi huo umesimama huku wananchi wakishindwa kupata huduma stahiki katika hospitali hiyo.
Aidha, Mhe. Mathayo amemuomba Mhe. Dkt. Nchimbi kufuatilia uanzishwaji wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJUNUAT) Butiama katika eneo la Hospitali hiyo ambapo tayari ekari 20 zimetengwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya chuo hicho.
Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sospiter Muhongo amesema ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere uliasisiwa na viongozi wa TANU miaka ya 1975 wakiwa na lengo la kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda.
Prof. Muhongo amesema mradi huo baadaye ulipelekwa Serikalini na kwa sasa unatoa huduma nzuri kwa wananchi na ukikamilika mapema utaokoa maisha ya wananchi wa Mkoa wa Mara na maeneo jirani.
Amemuomba Mhe. Nchimbi kufuatilia suala la kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Tiba katika eneo hilo ambalo amesema limechukua muda mrefu kuanza kutekelezwa.
Katika ziara hiyo, Mhe. Nchimbi ameambatana na viongozi na Watendaji wa CCM na Serikali na kauli mbiu ya miaka 61 ya Muungano ni “Muungano wetu ni Dhamana, heshima na tunu ya Taifa, Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.