Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko anategemewa kuwaongoza waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga yatakayofanyika tarehe 16 Aprili, 2025 katika eneo la Mikungani, Wilaya ya Bunda.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhani msiba wa Mhandisi Nyamohanga, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi amesema marehemu NyamoHanga alikuwa mzalendo na mpenda maendeleo ya nchi na kifo chake ni msiba mkubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Mara na Watanzania.
“Mhandisi Nyamohanga alikuwa mdau mkubwa wa maendeleo wa Mkoa wa Mara na ametusaidia sana katika kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kusambaza umeme katika vitongoji vya Mkoa wa Mara na maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo ambayo awali yalikuwa hayapati umeme.
Mhe. Mtambi amesema Mhandisi amesaidia pia kupeleka umeme katika Shule ya Amali ya Mkoa inayoendelea kujengwa katika Wilaya ya Butiama na amesaidia pia kurejesha umeme kwa haraka wakati wa maafa yaliyosababishwa na mvua ya upepo yaliyotokea Manispaa ya Musoma kwa kuhakikisha TANESCO inarejesha umeme eneo lililoathirika haraka.
Mhe. Mtambi ametoa pole kwa viongozi na watendaji wa Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Wizara ya Nishati, TANESCO na wafiwa wote wanaohusika katika msiba huo na kuwataka waombolezaji kuendelea kumuenzi Mhandisi Nyamohanga kwa kutenda mambo mazuri kwa Taifa letu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanda ya Ziwa wa TANESCO Mhandisi Satco Nombo amesema kwa sasa maandalizi muhimu kwa ajili ya mazishi ya Mhandisi Nyamohanga katika eneo la Migungani, Wilaya ya Bunda yanaendelea vizuri.
Mhandisi Nyamohanga amesema viongozi, menejimenti na watumishi kutoka TANESCO na Wizara ya Nishati, taasisi nyingine za Serikali na wanafamilia wanaotarajiwa kushiriki mazishi hayo wanatarajiwa kufika Bunda kuanzia tarehe 15 Aprili, 2025.
Mhandisi Nombo amesema aliyekuwa Dereva wake ambaye pia alifariki katika ajali hiyo Ndugu Mujahir Mohamed Haule tayari amesafirishwa kwenda Mkoa wa Pwani na amezikwa tarehe 14 Aprili, 2025.
Mhandisi Nyamohanga na dereva wake walifariki katika ajali iliyotokea usiku wa kuamkia tarehe 13 Aprili, 2025 katika Kata ya Nyatwali, jirani na geti kuu la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti lililopo eneo la Ndabaka, Wilaya ya Bunda.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Kamati ya Usala ya Wilaya ya Bunda, baadhi ya watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.