Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 01 Machi, 2025 ameongoza hafla ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara kuwatunuku askari waliofanyakazi nzuri kwa mwaka 2024 iliyofanyika katika viwanja vya Field Force, Manispaa ya Musoma ambapo amewataka wanasiasa wa Mkoa wa Mara kufanya siasa zao kwa kuzingatia amani na utulivu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mtambi amesema Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara imejiandaa vizuri kwa ajili ya kusimamia amani na utulivu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na haitamvumilia mtu yoyote anayefanya siasa potoshi, kutoa matamko yanayochochea uvunjifu wa amani na kuvuruga amani na utulivu uliopo katika Mkoa.
“Wale wote watakaopandwa na homa ya uchaguzi bila kujali vyama vyao vya siasa, Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara itawapa sindanao na dawa stahiki ili kushusha homa hiyo kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo” amesema Mhe. Mtambi na kuwahakikishia wanasisasa wanaopenda amani na utulivu kuwa watafanya shughuli zao katika mazingira salama.
Mhe. Mtambi amewataka watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kuacha kujiingiza kwenye masuala ya kisiasa na kuwataka kufuata taratibu zinazowaruhusu kupiga kura na kuchagua viongozi mbalimbali wanatakaoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kanali Mtambi amelipongeza Jeshi la Pilisi Mkoa wa Mara kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwapongeza askari wote waliopewa vyeti vya heshima na zawadi kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuwataka kuendelea kufanyakazi na kuiishi kauli mbiu yao ya Nidhamu, Haki, Weledi na Uadilifu ili amani na usalama uliopo Mkoa wa Mara uendelee kutamalaki.
Aidha, amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Mara wanaotoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kuwataka wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano ili kuuweka Mkoa wa Mara kuwa ni sehemu salama kwa shughuli za uchumi na maendeleo na kuweza kuvutia wawekezaji na watalii zaidi.
Mhe. Mtambi amewapongeza wadau malimbali wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara ambao wamekuwa wakisaidia jitihada mbalimbali za jeshi hilo katika kusimamia amani na usalama wa wananchi na mali zao na kuwataka wadau hao kuendelea kuliunga mkono Jeshi la Polisi na kutoa ushirikiano.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (ASP) Pius Lutumo amesema zoezi la kuwatambua askari na wadau waliofanya vizuri lipo kwa mujibu wa taratibu za Jeshi hilo na taratibu za kawaida za Utumishi wa Umma.
ASP Lutumo amesema askari na wadau waliotunukiwa leo wamefanyakazi nzuri kwa Jeshi la Polisi katika mwaka 2024 na kuwa askari wote wamepewa vyeti na pesa taslimu shilingi 500,000 kila mmoja na kuwapongeza wote waliofanikiwa kutunukiwa zawadi hizo.
Kamanda Lutumo amesema utoaji wa zawadi hizi ni tafsiri ya Inspekta Generali wa Polisi (IGP) kuhusiana na maelekezo yanayotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusiana na kuwapa askari mafunzo kazini, motisha wanapofanyakazi nzuri na kuendelea kuwapunguza askari wanaolitia doa jeshi hilo.
Mhe. Mtambi akiwa katika hafla hiyo mbali na kuzungumza na askari, amekagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili ya hafla hiyo, amewatunukia vyeti vya heshima na zawadi baadhi ya askari waliofanya vizuri na wadau wa Jeshi la Polisi Mara na kuangalia maonyesho ya vikosi mbalimbali vya Jeshi la Polisi.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Kamati ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Mara, wadau mbalimbali na askari pamoja na familia zao.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.