Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo tarehe 14 Aprili, 2025 amezindua mradi wa madawati, viti na meza kwa shule za Wilaya ya Tarime kupitia fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) zilizotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara katika Sekondari ya Ingwe, Nyamongo, Tarime.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Mtambi ameupongeza Mgodi huo kwa kutekeleza kwa haraka agizo alilolitoa mwishoni mwa Februari, 2025 wakati akiwa katika ziara ya kukagua miradi katika katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambapo alishuhudia wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyanungu kiwa wamekaa chini.
“Nimekagua madawati na meza na viti, nimekalia na nimejiridhisha yapo katika ubora unaotakiwa hongereni sana kwa kutekeleza mradi huu kwa wakati” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewapongeza Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa kuwa mfano wa kuigwa baada ya kupokea mabadiliko ya sheria na kanuni za madini na kuandaa mpango wa matumizi ya fedha za CSR kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mhe. Mtambi amewataka wasimamizi wa miradi ya CSR kuhakikisha wanatumia vizuri fedha hizo na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ili kuboresha hali ya kimaisha katika vijiji vinavyouzunguka mgodi na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Meja Edward Gowelle ameupongeza mgodi huo kwa kuanza kutekeleza miradi 101 ya CSR na kuanza na madawati kutokana na upungufu mkubwa wa madawati uliokuwepo katika shule za msingi na Sekondari za Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Meja Gowelle amesema Wilaya ya Tarime imekubaliana na mgodi kuwa kila wiki madawati yanayoendelea kutengenezwa na wazabuni wanne waliopewa zabuni na mgodi wa North Mara yatakuwa na kusambazwa katika shule mbalimbali za Wilaya ya Tarime.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tarime Vijijini Mhe. Mwita Waitara ameupongeza mgodi wa Barick North Mara kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa viongozi na wananchi wa Tarime na hususan vijiji 11 vinavyouzunguka mgodi huo.
Mhe. Waitara amesema mgodi kwa sasa unatekeleza miradi mingi ya kijamii tofauti na awali kabla yeye hajawa mbunge wa jimbo hilo na umetoa shilingi bilioni 21.2 kama mrahaba kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Mhe. Waitara ameushukuru Mgodi kwa kuanza kutoa mrabaha wa asilimia moja ya faida kwa vijiji vitano ambavyo vina uchimbaji baada ya Mgodi kufanya mazungumzo na vijiji hivyo kuanzia miaka ya 1995/1996 bila ya mafanikio.
Aidha, ameushukuru mgodi kwa kutoa sehemu ya lesseni zake na kuvigawia vikundi vya vijana jambo ambalo amesema litapunguza vijana wasio na ajira katika eneo hilo na kupunguza uvamizi wa vijana katika mgodi.
Mhe. Waitara amesema kuna hatua kubwa sana ya maendeleo katika jimbo hilo wakati huu ukilinganisha na wakati anaingia kama Mbunge wa jimbo hilo.
Mhe. Waitara amechukua fursa hiyo kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi na Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Meja Edward Gowelle kwa kazi nzuri wanazozifanya katika Mkoa wa Mara na Wilaya ya Tarime.
Awali akitoa taarifa, Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Ndugu Apolinary Lyambiko amesema Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ilipitisha miradi 101 itakayotekelezwa katika kata zote 26 za Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa kutumia fedha za CSR za mwaka 2022/2023 kwa gharama ya shilingi 9,049,264,380.00.
Bwana Lyambiko amesema kati ya miradi yote ya CSR, miradi 18 imekamilika, miradi mingine inaendelea na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwemo mradi wa madawati ambao unazinduliwa katika hafla hiyo.
Ndugu Lyambiko amesema katika mpango wa matumizi ya CSR, Halmashauri kwa kushirikiana na mgodi huo wanatarajia kutengeneza madawati 5,765 na seti za viti na meza 3,647 mpango huo utakapokamilika.
“Leo katika tukio hili, tunakabidhi madawati 890 na seti za viti na meza 295 kama zilivyowasilishwa na wakandarasi waliopewa zabuni ya kuziandaa samani hizo” amesema Bwana Lyambiko.
Bwana Lyambiko amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuweza kutenga muda wake na kushiriki uzinduzi wa ugawaji wa madawati hayo na kueleza kuwa samani hizo zimeanza kutolewa tarehe 29 Machi, 2025 na kusambazwa katika baadhi ya shule na wanategemea kukamilisha zoezi hilo mwishoni mwa Aprili, 2025.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.