Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao cha Kamati ya Barabara ya Mkoa wa Mara ambacho kimejadili taarifa ya utekelezaji wa matengenezo ya barabara kuanzia mwezi Julai 2024 hadi Desemba 2024 na kutoa siku 21 kuondolewa kwa vituo vya mabasi vya DDH na Nyasura katika Mji wa Bunda.
“Ninawataka Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Jeshi la Polisi na wadau wengine wote kuhakikisha mabasi ya abiria yanaingia stendi ya Mji wa Bunda na kuacha kushusha abiria katika vituo hivyo ili kupunguza ajali katika eneo hilo” amesema Mtambi.
Mhe. Mtambi ametoa kauli hiyo kufuatia ombi la wajumbe kutaka magari yote ya abiria na hususan yanayotokea Mwanza kuingia katika stendi ya Mji wa Bunda ili kupunguza ajali na kuongeza mapato ya Halmashauri.
Mhe. Mtambi amesema baada ya hapo Jeshi la Polisi liwachukulie hatua madereva wote watakaokaidi kutekeleza mabadiliko hayo ili kuokoa maisha ya abiria na wananchi wa maeneo hayo.
Mhe. Mtambi amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya kuitafutia ofisi Wakala wa Barabara wa Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mara na kuwaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzitafutia ofisi TARURA katika maeneo yao.
“Ninatoa mpaka Juni, TARURA wawe wamepatiwa ofisi katika majengo ya Serikali yaliyopo katika Mkoa na Wilaya ili kuboresha mazingira yao ya kufanyiakazi” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kutoka TARURA kuwa wakala hiyo haina ofisi katika maeneo mengi na inalipa gharama kubwa kupanga majengo ili kutoa huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Mara.
Akiwasilisha taarifa ya Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mara Mhandisi Maribe Vedastus Maribe amesema katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Desemba 2024 TANROADS kupitia mizani za Sirari, Rubana na Nyantare imepima uzito wa jumla ya magari 80,345 na kati ya hayo magari 236 yalizidisha uzito na kutozwa faini ya jumla ya shilingi 117,135,348.
Mhandisi Maribe amesema changamoto waliyokutana nayo katika utekelezaji wa miradi ya barabara katika kipindi hicho ni ufinyu wa bajeti inayotolewa ukilinganisha na mahitaji halisi, fedha za matengenezo ya barabara na usimamizi wa kazi kutotolewa kwa wakati, changarawe kwa ajili ya matengenezo ya barabara kupungua maeneo mengi na kusababisha gharama za matengenezo kuongezeka.
Bwana Maribe amesema changamoto nyingine ni hujuma za miundombinu barabarani ikiwemo wizi na uharibifu wa alama za barabarani, taa za barabarani, vyuma vya madaraja na makalavati na mifugo kutembezwa barabarani.
Mhandisi Maribe amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 jumla ya shilingi 15,312,692,000 zimeombwa kutoka Mfuko wa Barabara kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 1,508.95 pamoja na matengenezo ya madaraja 76.
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2025/2026 TANROADS imeomba kutoka Mfuko wa Barabara na Serikali Kuu jumla ya shilingi 226,851,410,000.00 kugharamia ukarabati, ujenzi wa kiwango cha lamo na usanifu wa barabara zenye jumla ya kilomita 320.31.
Katika kikao hicho wajumbe wamepitisha azimio la kuipandisha hadhi barabara ya Busabara –Mugara iliyopo katika Wilaya ya Bunda iliyokuwa inahudumiwa na TARURA ili iweze kuhudumiwa na TANROADS Mkoa wa Mara.
Katika kikao hicho wabunge waliohudhuria wamepongeza utendaji wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara Mhandisi Vedastus Maribe na kuiomba Serikali kukamilisha barabara mbalimbali zinazojengwa katika Mkoa wa Mara.
Kikao cha kamati ya Barabara kimehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, wabunge, wevyeviti na wakurugenzi wa Halmashauri, Meneja wa Mkoa wa TANROADS, Meneja wa Mkoa na Wilaya wa TARURA, SUMATRA, TEMESA na wadau wengine wa barabara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.