Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo tarehe 14 Aprili, 2025 amezungumza na wananchi wa Nyamongo wakati wa hafla ya uzinduzi wa amani na kukemea vitendo vyote vya uvunjifu wa amani katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Mtambi amesema Kamati ya Usalama ya Mkoa na Wilaya zipo imara kufuatilia matukio yote ya uvunjifu wa amani na hususan wakati huu tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kuwatahadharisha watu wote wanaopata kufanya vurugu na uchochezi katika Mkoa wa Mara.
“Ninaomba kuwatahadharisha wale wote wanaotaka kufanya vurugu katika Mkoa wa Mara, kitakachowapata hawataamini na tutakabiliana nao na tutawachukulia hatua za kisheria” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewaonya watu wanaovamia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kuwa asilimia 16 ya hisa zote za Mgodi huo zinamilikiwa na Serikali na kwa maana hiyo sehemu ya mgodi huo ni mali ya Watanzania na kama Mkoa hautakuwa tayari kuacha wavamizi waendelee kuvamia mgodi huo kila wakati.
Aidha, amewataka wananchi wanaotakiwa kuhama kupisha maendeleo ya mgodi huo wachukue fidia zao kabla hawajafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kukwamisha utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa kuzuia upanuzi wa shughuli za mgodi huo.
Mhe. Mtambi ametumia pia fursa hiyo kukwakemea wanasiasa wanaofanya siasa za upotoshaji, uchochezi na chokochoko zisizo na maana katika Mkoa wa Mara.
Akiwa katika eneo hilo pia alisikiliza kero za wanafunzi wa Shule za Msingi Kewanja na Shule ya Sekondari ya Ingwe na kutoa siku 14 kwa Mkuu wa Wilaya kuhakikisha maji ya uhakika yawe yamefika katika Shule ya Msingi Kewanja na kuuagiza mgodi wa Barrick North Mara kupeleka maji ya boza na matenki ya kuhifadhia maji katika shule hiyo kuanzia tarehe 15 Aprili, 2025.
Aidha, amemwagiza Mkuu wa Wilaya kufuatilia suala la umeme kukatika mara kwa mara katika Shule ya Sekondari Ingwe na kutoa siku 14 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuandaa mpango wa kuongeza mabweni katika shule hiyo.
Mhe. Mtambi amemwagiza Afisa Elimu Mkoa wa Mara na Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwenda Dodoma kufuatilia vitabu kwa ajili ya masomo ya Sanaa kwa kidato cha tano na cha sita na kutoa mrejesho kwake kuhusu upatikanaji wa vitabu katika shule hiyo.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Meneja Mkuu wa Mgodi huo Bwana Apolinary Lyambiko amesema katika mpango wa kupanua shimo la Nyabilama hadi tarehe 14 Aprili, 2025 watu 593 kati ya 728 wameshapokea fidia zao huku watu 135 hawajajitokeza kupokea fidia jambo ambalo linakwamisha mgodi huo kuanza kupanua shimo hilo.
Bwana Lyambiko amesema watu 37 kati ya wote waliochukua fidia zao wamechagua fidia mbadala tofauti na fedha na mgodi umetekeleza kulingana na matakwa ya wanaofidiwa kulingana na taratibu za kisheria.
“Bado kuna watu 11 ambao walipaswa kufidiwa wamekataa kufanyiwa uthamini licha ya kuzungumza nao mara kwa mara kuhusiana na umuhimu wa wao kuhama kupisha utekelezaji wa shughuli za mgodi katika eneo hilo” amesema Bwana Lyambiko.
Aidha, Bwana Lyambiko ameelezea wasiwasi wake kuwa kutokana na kipindi cha mvua na kampeni za kisiasa wavamizi katika mgodi huo wanaweza kuongezeka zaidi wakati jitihada mbalimbali zilizokuwa zimefanyika zilifanikiwa kuwapunguza wavamizi hao kwa kiasi kikubwa.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.