Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 14 Aprili, 2025 amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Wilaya ya Serengeti katika Kijiji cha Makundusi, Wilaya ya Serengeti na kukemea vitendo vya ukabila miungoni mwa viongozi na wananchi.
Mhe. Mtambi amekemea vitendo hivyo baada ya kusikiliza kero za wananchi na katika mkutano wa hadhara baada ya kupokea baadhi ya kero zinazozungumzia utengano wa viongozi na wananchi kwa kufuatana na ukabila katika eneo hilo.
“Ndugu zangu ninaomba tubadilike, katika kikao chetu hapa yamejitokeza mambo yanayohusu ukabila, niwaambie tu ukabila haujengi wala hauna manufaa yoyote kwa maendeleo yenu. Tuwakemee wote wanaoendekeza ukabila hata kama ni viongozi wetu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi kupendana na kusaidia ili kuishi kwa amani na utulivu na kuacha tabia za kujichukulia sheria mkononi, mila potofu na vitendo visivyofaa katika jamii ambavyo amesema vitarudisha nyuma maendeleo yao.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi kuukata ukabila kwa sababu hauna mwisho mzuri na kutanguliza Utanzania wao na kwa kufanya hivyo wanaweza kujifunza na kuishi kwa amani kwa watu wa makabila mengine na kujiletea maendeleo yao na familia zao.
Kanali Mtambi amesema nchi inapoelekea katika uchaguzi, wananchi wawaogope viongozi wanaowagawa kutokana na makabila yao bali wawachague viongozi wanaowaunganisha na kupigania maendeleo ya wananchi wote.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi kushiriki uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kuwachagua viongozi wanaopenda maendeleo na kuachana na wanaofanya siasa za uchochezi, ukabila na ugombanishi.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara amesikiliza kero, changamoto na ushauri kutoka kwa wananchi na kutoa maelekezo mbalimbali kutatua kero na changamoto za wananchi wa eneo la Makundusi.
Aidha, ili kutatua kero hizo, Mhe. Mtambi ametoa maagizo mbalimbali kwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Kijiji cha Makundusi na taasisi za Grumeti, RUWASA na kadhalika.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Kamati ya Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Serengeti, Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na wawakilishi wa taasisi za umma na binafsi zilizopo Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.