Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 11 Aprili, 2025 amefanya ziara katika Wilaya za Musoma na Tarime kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kuwakemea watendaji kuhusu michakato isiyoisha katika utekelezaji wa miradi.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara hiyo, Mhe. Mtambi amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati ili miradi hiyo iweze kutoa huduma zilizopangwa kwa wananchi.
“Sitaki kusikia habari za michakato isiyoisha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mara, kamilisheni miradi ya maendeleo kwa wakati ili huduma zitolewe katika miradi hiyo” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema awali, tatizo lilikuwa upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi, kwa sasa Mheshimiwa Rais ameleta fedha za kutekeleza miradi lakini michakato inafanyika taratibu na kukwamisha utekelezaji wa miradi kwa wakati na kusababisha wananchi kukosa huduma inayotarajiwa na Mhe. Rais wakati analeta fedha.
Aidha, amewataka watendaji kuacha kutumia kisingizio cha ugumu wa matumizi ya mfumo wa Manunuzi Serikalini (NEST) baada ya kuchelewesha kukamilisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwahakikishia kuwa mfumo upo vizuri na Halmashauri nyingine zinafanya vizuri katika matumizi ya mfumo huo.
Wakati huo huo, Mhe. Mtambi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wingi katika Mkoa wa Mara tangu alipoingia madarakani.
“Mkoa wa Mara tumependelewa kwa kupewa miradi mingi ya kimkakati, ambayo ikikamilika itaufanya Mkoa na wananchi wake kupiga hatua kubwa sana kimaendeleo” amesema Mhe. Mtambi.
Akiwa katika Wilaya ya Musoma, Mhe. Mtambi amekagua ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma wakati akiwa Tarime ametembelea ujenzi wa Shule ya Sekondari Mpya ya Kibumaye na kutembelea na kuzungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mogabiri.
Aidha, Mhe. Mtambi amekagua na kutembelea mradi wa barabara ya Mogabiri- Nyamongo (KM 25) inayojengwa kwa kiwango cha lami ikiwa ni sehemu ya barabara ya Tarime- Mugumu, amekagua mradi wa upanuzi wa miundombinu katika Shule ya Sekondari ya Julius Kambarage Nyerere.
Mhe. Mtambi amehitimisha ziara yake kwa kumtembelea Mkandarasi mzawa Isack Charles Wange ambaye ni mmiliki wa RIN Contractors and General Supply Campany Limited ofisini kwake katika eneo la Nyamongo ambaye ni mdau muhimu wa maendeleo ya Wilaya ya Tarime.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mtambi ameambatana na Wakuu wa Wilaya za Musoma na Tarime, Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, TANROADS, TAA, Halmashauri ya Tarime na Wakandarasi na wazabuni wanaotekeleza miradi hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.