Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo tarehe 26 Februari, 2025 amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kutembelea Shule ya Sekondari ya Nyanungu na Sekondari Mpya inayojengwa katika Kijiji cha Kegonga na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Akizungumza katika Shule ya Sekondari Nyanungu alipoenda kukagua mradi wa maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha tano, Mhe. Mtambi amesema mradi huo umechelewa sana kutekelezwa pamoja na kwamba fedha za mradi huo zilipokelewa kuanzia Machi, 2024.
“Sasa tunakaribia mwaka mmoja tangu fedha za mradi huu mlipopokea lakini baadhi ya majengo (mabweni mawili) yapo kwenye msingi na mengine yanaendelea kukamilishwa kwa kasi ndogo, hii haikubaliki kabisa” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesikitishwa na kitendo cha wanafunzi wa Sekondari hiyo kukosa madawati ya kuwatosheleza huku Halmashauri ikisema imetenga bajeti ya ununuzi wa madawati katika fedha za CSR zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
Mhe. Mtambi ametoa hadi tarehe 30 Machi, 2025 Shule zote za Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ziwe zimepata madawati ya kutosheleza idadi ya wanafunzi waliopo na kuionya Halmashauri hiyo kuwa atasimamisha malipo ya stahili za Mkurugenzi na posho za Baraza la Madiwani mpaka wanafunzi watakapopata madawati.
Aidha, Mhe. Mtambi amesema hajaridhishwa na ubora wa umaliziaji katika majengo hayo na kuwataka wasimamizi wa mradi wa ujenzi kuwasimamia vizuri mafundi wanaojenga majengo hayo kukamilisha kazi vizuri bila kulipua.
Kanali Mtambi ameitaka Taasisi ya Kudhibiti na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara kufuatilia utoaji wa zabuni ya kuleta tofali katika miradi hiyo ili kujiridhisha na taarifa kuwa mzabuni huyo amepewa zabuni katika miradi mingi ya Serikali huku akiwa hana uwezo wa kuzalisha matofali ya kutosha kwa wakati.
Wakati huo huo, Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya kuwakamata wazazi wa wanafunzi wanaotakiwa kwenda shule ambao hawajasajiriwa mpaka sasa na hawatoi ushirikiano kwa watendaji wanaowafuatilia wanafunzi hao na kuwafikisha mahakamani.
“Wanafunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza ni lazima waende shule na hakikisheni hamna mzazi au mlezi wa mtoto anayeacha kumpeleka mtoto shule na kugoma kutoa ushirikiano kwa watendaji anaachwa” amesema Mhe. Mtambi.
Akizungumza katika ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Bibi Pelagia Balozi amesema Halmashauri hiyo imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya ununuzi wa madawati kwa ajili ya shule zote za Halmashauri zenye upungufu hata hivyo mchakato wa manunuzi bado unaendelea.
“Mgodi umetuhakikishia kuwa mwezi Machi, 2025 wazabuni watakuwa wamepatikana na kuanza kazi ya kutengeneza madawati hayo pamoja na manunuzi mengine ya miradi ya CSR itakayotekelezwa” amesema Bibi Balozi.
Bibi Balozi amesema awali mchakato wa zabuni ulifika sehemu ukaanza upya baada ya Mgodi wa North Mara kubadilisha taratibu zake za manunuzi na hivyo kulazimisha zabuni hizo kuanza upya na kuathiri upatikanaji wa madawati na utekelezaji wa miradi ya CSR katika Halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Nyanungu Mwalimu Casmiry Emmanuel Kanga ambaye pia ni msimamizi Mkuu wa Sekondari mpya ya Kegonga amesema Shule ya Sekondari Nyanungu ilipokea shilingi 555,586,099.47 kutoka Serikali Kuu, mradi wa SEQUIP na EP$R kwa nyakati tofauti tofauti kuanzia Machi, 2024 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kidato cha tano na sita.
Mwalimu Kanga amesema miundombinu inayojengwa ni pamoja na vyumba vya madarasa saba, matundu matundu 30 ya vyoo, mabweni mapya matatu na ukailishaji wa bweni moja na mradi huo uko katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.
Bwana Kanga amesema mpaka sasa jumla ya shilingi 232,680,484.29 zimetumika kulipa wazabuni walioleta vifaa na mafundi na malipo ya vifaa vyenye thamani ya shilingi 64,041,689.44 yapo kwenye mchakato wakati fedha iliyobakia ni shilingi 258,863,925.74.
Aidha, Mwalimu Kanga amesema Shule ya Sekondari Nyanungu ilipokea shilingi milioni 584 mwezi Juni, 2024 kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari Mpya katika Kijiji cha Kegonga na utekelezaji wa mradi ulianza Oktoba, 2024 na mpaka sasa majengo mengi yapo katika hatua ya ukamilishaji huku majengo mawili yapo katika hatua ya boma.
Mwalimu Kanga amesema miradi hiyo imechelewa kutekelezwa kutokana na ucheleweshaji wa mzabuni wa tofali ambaye amechukua zabuni katika miradi mingi ya Serikali na anashindwa kuwasilisha matofali kwa wakati.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mtambi amezungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyanungu, Shule ya Msingi Kegonga na wananchi wa Kata ya Nyanungu katika mradi mpya wa Sekondari ya mpya ya Kegonga na kuwasikiliza wananchi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mtambi ameongozana pia na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, viongozi na watendaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.