Mkoa wa Mara umezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) pamoja na wadau wote wa sekta ya elimu kushirikiana na Serikali katika kutatua kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Vincent Naano Anney amesema hayo leo tarehe 20 Februari, 2025 wakati akifungua rasmi Kliniki ya Kusikiliza Kero za Walimu Mkoa wa Mara iliyofanyika katika ukumbi wa uwekezaji na kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga siku maalum ya kuendelea kusikiliza kero na changamoto za walimu.
“Wakurugenzi wa Halmashauri waanzishe siku maalum ya kusikiliza na kutatua kero za walimu ili kutoa mwendelezo wa utatuaji wa kero za walimu katika halmashauri zote za Mkoa wa Mara baada ya zoezi la leo kuwa limehitimishwa” amesema Dkt. Anney.
Dkt. Anney amesema pamoja na Serikali kuchukua hatua mbalimbali kutatua kero za walimu, bado walimu wengi wanachangamoto na hivyo utatuzi wa kero hizo unapaswa kuwa endelevu kwa wadau wote kushirikiana kutatua kero za walimu.
Dkt. Anney amezitaja hatua ambazo Serikali imezichukua kutatua kero za walimu kuwa ni pamoja na kuwapandisha madaraja, kuongeza mishahara, kujenga nyumba za walimu na kuboresha miundombinu ya kujifunza na kufundishia ambayo imewasaidia walimu kufanyakazi katika mazingira mazuri.
Dkt. Anney ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda amekitaka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kushirikiana na Benki ya Walimu Tanzania kutumia kliniki ya Kutatua Kero za Walimu kuwapa walimu elimu kuhusu masuala ya fedha na uchumi ili walimu waweze kuboresha maisha yao.
Aidha, ameitaka Benki ya Walimu kuona namna bora ya kuwasaidia walimu kwa kufungua matawi ya benki hiyo katika ngazi za Mikoa na Wilaya, kuwapa elimu ya fedha na kutoa mikopo yenye riba nafuu ili kuwakwamua walimu kiuchumi na hususan wanaoishi kwenye mazingira ya vijijini.
Dkt. Anney amezishukuru Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Tume ya Utumishi wa Walimu, Wizara ya Fedha kwa kuona umuhimu wa zoezi hilo na kutoa maafisa waandamizi kushughulikia na kutatua kero za walimu.
Dkt. Anney amewataka walimu wa Mkoa wa Mara kutumia fursa hiyo kuwasilisha kero zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi na baada ya hapo warudi kwenda kutekeleza majukumu yao wakati Serikali inaendelea kushughulikia kero walizowasilisha.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya amewataka walimu wa Mkoa wa Mara kutumia siku hii vizuri kwa kuwasilisha kero, changamoto mbalimbali zinazowakabili ili ziweze kutatuliwa.
“Leo wataalamu wote wanaohusika kutatua kero wapo hapa, tutumie fursa hii vizuri katika kutatua kero na changamoto mbalimbali, hasa zile kero kubwa zinaweza kupata dawa hapa” amesema Bwana Kusaya.
Aidha, Bwana Kusaya amewataka walimu kuendelea kuwasilisha kero zao kama kawaida na zile ambazo wanaona Halmashauri hazifanyii kazi waziwasilishe Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa ajili ya kupatiwa utatuzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Mara Bwana Abdallah Malima amewashukuru viongozi wa CWT na wataalamu wote wanaohusika katika kufanikisha Kliniki hiyo ya kutatua kero za walimu.
Mwalimu Malima pia amewashukuru walimu wa Mkoa wa Mara kwa mwitikio wao kuja kupatiwa ufumbuzi wa kero na changamoto zao zinazowakabili na kuwataka kutoa ushirikiano kwa wataalamu ili kero zao ziweze kutatuliwa.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa CWT Taifa Bwana Selemani Ikomba amewashukuru viongozi, wataalamu na walimu wa Mkoa wa Mara waliojitokeza kushiriki katika Kliniki hiyo na kuwataka walimu kutumia fursa hiyo vizuri.
“Tangu tumepata Uhuru hii ni mara ya kwanza walimu tunakusikilizwa kero zetu kwa mfumo wa namna hii, tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa maono yake mazuri” amesema Bwana Ikomba.
Bwana Ikomba amesema tayari Kliniki hiyo imeshapita katika mikoa 17 hapa nchini na baada ya Mkoa wa Mara itakuwa imebakisha Mikoa nane kati ya mikoa 26 iliyopo na kote walikopita wamepata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi wa Serikali, Walimu na wadau wengine.
Kwa upande wake, Bi. Judith Bosco Abdallah Afisa Utumishi Mkuu kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni kiongozi wa wataalam wa Serikali wanaosikiliza kero za walimu amesema Kliniki hiyo imehusisha wataalamu kutoka Wizara mbalimbali ili kutatua kero za walimu.
Bi. Abdallah amesema katika mikoa 17 waliyopita mpaka sasa, kero kubwa za walimu walizokutana nazo ni kutopandishwa madaraja, malimbikizo ya mshahara, madai mbalimbali, watumishi kujiendeleza na kutopandishwa madaraja kwa wakati na kadhalika.
Amesema baada ya Kliniki hiyo watafanya kikao cha tathmini na Mkoa utapewa nafasi ya wiki mbili kufanyia kazi changamoto zitakazobainika katika zoezi hilo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.