Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Dominicus Lusasi leo tarehe 28 Februari, 2025 amezindua Mpango Shirikishi wa Uvuvi Salama katika Kijiji cha Busekela, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma uliofadhiliwa na Shirika lisilo la kiserikali la EMEDO na kuliomba shirika hilo kupeleka elimu ya kuzuia kuzama maji katika Wilaya nyingine za Mkoa wa Mara zinazozunguka ziwa Victoria.
Akizungumza kabla ya uzinduzi wa mpango huo, Bwana Lusasi amesema ajali za majini zinesababisha watu wengi kupoteza maisha na kuwa chanzo cha familia nyingi kuishi maisha duni kwa kupoteza nguzo muhimu katika familia zao.
“Eneo kubwa la Mkoa wa Mara linazungukwa na Ziwa Victoria na mradi huu unavisaidia vijiji viwili tu vya Wilaya ya Musoma, kama itawezekana tunaomba mpanue huduma za mradi huu ili Wilaya zote zinufaike na mradi huu” amesema Bwana Lusasi.
Bwana Lusasi amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka watu 300,000 duniani hupoteza maisha kwa kuzama maji na zaidi ya asilimia 90 ya vifo hivyo vinatokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ikiwemo Tanzania.
Aidha, Bwana Lusasi amelitaka Shirika la EMEDO kuhakikisha kuwa majaketi okozi yanapatikana katika maeneo ya wavuvi na kwa kulipia kidogo kidogo ili kuwawezesha wavuvi kumiliki vifaa hivyo vya usalama katika maisha yao.
Bwana Lusasi ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kuendelea kutoa elimu kuhusu usalama wa majini na uokoaji kwa wavuvi kupitia mikutano ya hadhara katika maeneo ya wavuvi ili kuwawezesha kufahamu namna ya kujikinga na ajali na kutoa msaada wakati wa dharura.
Amewataka wananchi kuzingatia utabiri wa hali ya hewa na kuchukua tahadhari kabla ya kusafiri majini na kuwataka wamiliki wa vyombo vya majini kuzingatia sheria na taratibu zote za usalama kwenye maji kabla ya vyombo vyao kuanza safari.
Bwana Lusasi amewataka wananchi wa eneo hilo kuzingatia usafi, kujenga vyoo bora na kuvitumia ili kuweza kujilinda na magonjwa ya mlipuko yanayotokana na uchafu.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mhe. Charles Nyambita Magoma amelishukuru Shirika la EMEDO kwa kuvifikia vijiji hivyo viwili katika mradi wao na kuwaomba kuongeza vijiji zaidi ili wananchi waweze kupata elimu.
“Halmashauri yetu ina kata 21 na kati ya hizo Kata 18 zimeguswa na Ziwa Victoria na wananchi wa kata hizi bado hawajapata elimu ya namna ya kujilinda na kuzama majini kama wenzao wa Busekera na Kome” amesema Mhe. Magoma.
Aidha, Mhe. Magoma amewataka wavuvi na wananchi wote kwa ujumla kuzifuata sheria ambazo wamezitunga ili kudhibiti ajali za kuzama majini na kuwataaka wananchi wa vijiji hivyo kutoa elimu kwa wenzao kuhusu sheria hizo na taratibu za vijiji ili ziweze kuenea katika mialo mingine ya wavuvi wa Ziwa Victoria.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Wakili Anabu Shariph amesema katika mchakato wa kutunga sheria hizo maoni yote ya wadau yalizingatiwa na sheria hizo zilipita katika Kikao cha Kamati ya Menejimenti, Kamati ya Mipango na Fedha na hatimaye kuidhinishwa na Baraza la Madiwani.
Wakili Shariph amesema sheria hizo zipo kwa ajili ya kudhibiti na kuwaokoa wananchi kutokana na ajali mbalimbali za kuzama na namna wanavyoweza kujikinga kwa kufuata na kuzingatia sheria hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la EMEDO Bibi Editrudith Lukanga amesema mradi huo umeibuliwa umetokana na utafiti uliofanywa na shirika hilo na kwa sasa unatekelezwa katika Wilaya za Nyamagana na Ukerewe (Mwanza), Muleba (Kagera) na Musoma (Mara).
Bibi Lukanga amesema kwa Mkoa wa Mara mradi huu unatekelezwa katika Vijiji vya Busekera na Kome na mpaka sasa mradi huu umefanikiwa kutoa elimu kwa watu 1,300 na robo yao wakiwa ni wanawake na mwaka huu wanategemea kutoa elimu kwa wavuvi 400.
Aidha, Bibi Lukanga ameiomba Serikali kulipa kipaumbele suala la usalama wa majini katika mipango na bajeti zake ili kudhibiti ajali zinazotokana na uzembe na watu kutokuzingatia sheria na taratibu za usalama majini.
Bibi Lukanga amesema mradi huo utatoa elimu kwa wananchi, utasambaza majaketi okozi ya gharama nafuu na kulipa kwa awamu na kufunga mabango ya utabiri wa hali ya hewa ya kisasa ili wananchi waweze kutambua kabla ya kuanza shughuli za uvuvi.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi huo Bwana Arthur Wihabu Mugema amesema Shirika la EMEDO litasambaza majaketi okozi ambayo yatakuwa yanapatikana katika maeneo mbalimbali na wananchi watalipia kwa bei ya ruzuku shilingi 40,000.
“Ili kuwarahisishia katika malipo wavuvi, shirika litatoa majaketi haya kwa mkopo na mvuvi atatakiwa kulipia taratibu hadi atakapokamilika deni lake la jaketi okozi” amesema Bwana Mugema.
Bwana Mugema amesema shirika hilo pia litafunga mbao tano za taarifa za hali ya hewa ambapo mbao mbili zitafutwa katika Kijiji cha Komen a mbao tatu zitafungwa katika Kijiji cha Busekera ili kuwawezesha wavuvi kupata taarifa sahihi za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Aidha, Bwana Mugema amesema Shirika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali litaendelea kutoa elimu ya usalama majini na namna ya kufanya uokoaji kwa kushirkiana na wadau mbalimbali ikiwemo Jeshi la Polisi, Halmashauri na Serikali kwa ujumla.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.