Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi akiwa ameambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara ametembelea Soko la kimkakati la Kimataifa la Mazao linaloendelea kujengwa Sirari na kumtaka mkandarasi wa mradi huo kukamilisha mradi kwa wakati.
“Ninataka mradi huu ukamilike kwa wakati ili wakulima na wafugaji waanze kulitumia soko hili kuuza mazao yao kimataifa na wanunuzi wanaokuja nchini wapate sehemu nzuri ya kufanya biashara yao” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuhakikisha huduma za maji na umeme zinakuwepo katika eneo la mradi na kuanzisha utaratibu wa kuwapata wafanyabiashara watakaotumia soko hilo ili mradi ukikamilika tu uweze kuanza kufanyakazi kama ulivyokusudiwa.
Mhe. Mtambi ametumia fursa hiyo kumshukuru sana Mhe. Rais kwa kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati katika Mkoa wa Mara na kuwataka wananchi wa Wilaya ya Tarime kujivunia miradi ya masoko mawili ya kimataifa yanayoendelea kujengwa katika Wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele amesema awali aliwaagiza TANESCO kufanya tathmini ya kupeleka umeme katika eneo la mradi huo na baada ya tathmini hiyo TANESCO walileta gharama ya kupeleka umeme kuwa ni shilingi milioni 70.
“Kwa kuwa kiasi hiki hakikuwepo kwenye bajeti za Halmashauri, nimeiagiza Halmashauri kutenga fedha hiyo katika bajeti zake ili kuleta huduma ya umeme katika soko hilo” amesema Meja Gowele.
Aidha, Meja Gowele amesema huduma ya maji iliyopo jirani na mradi huo ipo kilomita moja kutoka katika mradi huo na RUWASA imeombwa kuangalia uwezekano wa kupeleka maji katika mradi huo.
Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi huo Mhandisi Samwel Mtaja akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara amesema mradi huo baada ya kusimamama kwa miaka 10 kwa sasa umeanza tena baada ya Serikali kumtafuta mkandarasi wa ukamilishaji wa mradi huo kwa gharama ya shilingi bilioni 1.4.
Mhandisi Mtaja amesema kwa sasa ujenzi wa mradi huo umefika asilimia 60 na kwa mujibu wa mkataba unategemea kukamilika Mei, 2025 na utakapokamilika utawafaidisha wakulima na wafugaji kwa kupata soko la uhakika la kimataifa la kuuzia mazao yao.
Mhandisi Mtaja amesema utekelezaji wa mradi huo unakabiliwa na changamoto mbili ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa huduma za maji na umeme katika eneo la mradi jambo ambalo linamfanya mkandarasi kufanya baadhi ya shughuli za mradi zinazohitaji umeme nje ya eneo la mradi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Bwana Simon Langoi akizungumza katika eneo la mradi huo amesema mradi huo unatekelezwa na Wizara ya Kilimo na ulianza katika mwaka wa fedha mwaka 2013/2014 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.3 lakini ulisimama mwaka 2014.
“Hata hivyo mradi huo ulisimama kwa takriban miaka 10 na sasa umeanza kutekelezwa tena baada ya Serikali kumpata mkandarasi wa ukamilishaji wa mradai huu” amesema Bwana Langoi.
Bwana Langoi amesema Halmashauri ya Wilaya ya Tarime imefanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kuhusu ukamilishaji wa mradi huo na kufanikiwa kuingizwa tena katika bajeti ya Wizara na kuanza kutekelezwa tena.
Soko la Kimkakati la Kimataifa la mazao linaendelea kujengwa katika Kijiji cha Lemagwe, Kata ya Lebicheri Tarafa ya Sirari na likikamilika litarahisisha biashara ya mpakani ya mazao kati ya nchi za Kenya na Tanzania.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Postal Address: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Telephone: +255282622305
Mobile:
Email: ras.mara@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Mara Region . All rights reserved.