Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Ndugu Gerald Musabila Kusaya leo tarehe 29 Mei, 2025 amefungua kikao cha Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSA) kwa mikoa ya mitatu ya Kanda ya Ziwa na kuwataka walimu kuwaongoza wanafunzi katika kufikia ndoto zao katika maisha.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho, Ndugu Kusaya amesema kuwa walimu ni kiungo muhimu katika maendeleo ya Taifa na kuwaahidi kuwa Serikali ya Awamu Sita itaendelea kuwa begabega na walimu wote hapa nchini Tanzania kutoka shule binafsi na za umma ili kufikia shabaha yake ya kumuinua Mtanzania.
“Muda wote walimu mpo shuleni mnawalea watoto wetu, kikao hiki mkitumie kubadilishana uzoefu wenu hasa kwa madarasa ya mitihani ili mikoa ya Kanda ya Ziwa Ifanye vizuri katika mitihani ya kitaifa” amesema Ndugu Kusaya.
Ndugu Kusaya amesema kuwa kuinua taalamu katika shule zote ndio kusudio la Serikali na kuwataka Wakuu wa Shule kuwasimamia vizuri walimu na wanafunzi ili waweze kufanya vizuri kitaaluma na hata kimichezo katika ngazi ya kitaifa.
Akizungumzia kuhusu upungufu wa walimu, ndugu Kusaya amesema kuwa shule nyingi zina changamoto ya uhaba wa walimu na kuongeza kuwa tatizo la uhaba wa watumishi siyo la walimu peke yao bali ni kada zote.
Bwana Kusaya amesema kwa sasa Mkoa wa Mara una upungufu wa watumishi 15,441 wa fani mbalimbali na Serikali imekuwa ikiongeza watumishi mara kwa mara ikiwemo walimu wa shule za msingi na sekondari.
Amewataka Wakuu wa Shule kuwa wabunifu kukabiliana na uhaba walimu kwa kutumia walimu wa ajira za muda mfupi wakati tatizo la uhaba wa walimu wakati linafanyiwa kazi na wamiliki wa shule hizo.
Katibu Tawala Mkoa amesema suala la uhaba wa walimu changamoto kubwa ni idadi ya watu imeoongezeka na kuibua uhaba wa watumishi na katika kukakabiliana na changamoto hiyo Serikali imekuwa ikitoa ajira mpya za watumishi kila mwaka.
Ndugu Kusaya amewataka Wakuu wa Shule kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula cha mchana shuleni kwa ushirikiano wa kamati za Shule, wazazi, viongozi na wadau na kuzitaka Halmashauri kutumia sheria ndogondogo kufanikisha suala hilo.
Aidha, amewahimiza wazazi na walezi kuwatunza watoto wao vizuri ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanapata chakula cha mchana wakiwa shuleni ili kuboresha ufaulu na utoro shuleni.
Ndugu Kusaya amewataka Wakuu wa Shule za Serikali kusimamia miradi katika maeneo yao kwa umakini na kuwapongeza kwa kusimamia vizuri miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAHOSA Kanda ya Ziwa alisema kuwa anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa maboresho ya sekta ya elimu kwa kutoa posho ya madaraka na elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita.
“Kumekuwa na ongezeko la walimu wanaoajiriwa, kulipwa madai mbalimbali, maboresho katika mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na maboresho ya mitaala” amesema Mwenyekiti wa TAHOSA.
Mwenyekiti huyu wa TAHOSA Kanda ameahidi kuwa wataongeza nguvu ya kuhamasisha wazazi/walezi kuhusu upatikanaji wa chakula cha mchana shuleni ili kuongeza ufaulu na kupunguza utoro.
Aidha, ameahidi kuongeza ushirikiano baina ya TAHOSSA Kanda ya Ziwa na serikali na kuongeza mafanikio zaidi ya kielimu na michezo.
Wakuu wa Shule wa Mikoa ya Geita, Mwanza na Mara walishiriki kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mwembeni Complex na kuhudhuriwa na wasimamizi wa sekta ya elimu Mkoa wa Mara na Wakuu wa Shule zaidi ya 700.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa