Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko leo tarehe 16 Aprili, 2025 amewaongoza waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Boniphace Gissima Nyamohanga yaliyofanyika katika eneo la Mikungani, Wilaya ya Bunda.
Akizungumza katika mazishi hayo, Mhe. Biteko amesema Mhandisi Nyamohanga alikuwa ni hazina kubwa ya mipango inayopimika ndani ya Serikali na amefanya kazi kubwa ndani ya TANESCO, REA na Wizara ya Nishati kwa ujumla.
Mhe. Biteko amesema kazi kubwa alizozifanya kuwa ni pamoja na ukamilishaji wa mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Nyerere na uanzishaji na utekelezaji wa mpango wa Tanzania kuanza kuuza umeme katika nchi ya Zambia.
“Sahihi yake aliyoiweka wakati wa kufunga mkataba kati ya Tanzania na Zambia itaendelea kuwepo katika mkataba huo muda wote kutukumbusha Kazi kubwa aliyoifanya Mhandisi Nyamohanga katika sekta ya Nishati” amesema Mhe. Biteko.
Naibu Waziri Mkuu amesema wakati Mhandisi Nyamohanga anateuliwa Shirika lilikuwa lipo katika wakati mgumu sana na kelele za umeme zilikuwa nyingi hapa nchini lakini ametatua tatizo la umeme na kujenga umoja na mshikamano baina ya watumishi wa TANESCO.
Mhe. Biteko amesema Mhandisi Nyamohanga alikuwa anawatetea na kuwapenda watumishi wake na wakati wote likitokea tatizo alikuwa anasema “wape muda watajirekebisha” amesema Mhe. Biteko na kuongeza kuwa marehemu alikuwa tayari kubeba lawama mbalimbali ili kuwasaidia watumishi wake.
Mhe. Biteko ametumia fursa hiyo kuwaasa waombolezaji wakiwemo viongozi na watendaji kuwa katika maisha yao waige mfano wa Mhandisi Nyamohanga na kuwa baraka ya kuwasaidia wengine na sio kuwa kama kitunguu kusababisha vilio kwa watu wanaomzunguka.
Mhe. Biteko amewataka wanafamilia ya Mhandisi Nyamohanga pamoja na wajane wawili wa marehemu kushikamana, kupendana na kuishi kwa umoja na amani kama wakati ambapo marehemu alipokuwa hai ili waweze kuendeleza maono ya marehemu katika maisha yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi amesema Mhandisi Nyamohanga alikuwa ni mdau muhimu sana katika Maendeleo ya Mkoa wa Mara na amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa kwa viongozi wa Mkoa wa Mara.
“Mhandisi Nyamohanga amefariki akiwa njiani pamoja na mambo mengine alikuwa anakuja kukagua na kuona namna ya kupeleka umeme katika Shule ya Amali ya Mkoa wa Mara inayoendelea kujengwa katika Wilaya ya Butiama” amesema Mhe. Mtambi.
Akizungumza katika mazishi hayo, Mhe. Mtambi ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara na Mkoa wa Kipolisi wa Tarime Rorya kuongeza operesheni na watu wote wanaokiuka taratibu za usalama barabarani wachukuliwe hatua za kisheria.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka viongozi, watumishi na wananchi kuiga mfano wa Mhandisi Nyamohanga kwa kuchapa kazi kwa bidii na kutatua kero za wananchi.
Kwa upande wake, Msemaji wa Familia ya Nyamohanga ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Mhe. Mwita Gachuma ameishukuru Serikali kwa uratibu mzuri wa mazishi ya Mhandisi Nyamohanga tangu msiba huo ulipotokea tarehe 13 Aprili, 2025
Mhe. Gachuma ameiomba Serikali kusaidia kujenga jengo kwa ajili ya kumkumbuka Mhandisi Nyamohanga katika eneo hilo alipozikwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sospiter Muhongo ambaye aliwahi kufanya nae kazi amesema Mhandisi Nyamohanga ni mmoja wa waanzilishi wa bei ya umeme ya 27,000 inayotumika hapa nchini kwa ajili ya kuunganishia umeme wa gharama nafuu na kuiwezesha Tanzania kuingia katika mradi wa Kimataifa wa Power Africa.
Prof. Muhonga ameiomba Serikali kumuenzi Mhandisi Nyamohanga na kutambuliwa kama mwanzilishi wakati wa tathmini ya mradi wa Power Africa itakayofanyika Juni, 2025 ili kukumbuka mchango wake mkubwa alioutoa katika Sekta ya Nishati.
Mhandisi Nyamohanga na dereva wake Ndugu Mujahir Mohamed Haule walifariki katika ajali iliyotokea usiku wa kuamkia tarehe 13 Aprili, 2025 katika Kata ya Nyatwali, jirani na geti kuu la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti lililopo eneo la Ndabaka, Wilaya ya Bunda na dereva wake alizikwa tarehe 14 Aprili, 2025 katika Mkoa wa Pwani.
Marehemu Nyamohanga alizaliwa mwaka 1969 na amefariki akiwa na umri wa miaka 56 na kuacha wajane wawili na watoto 15 na wajukuu watano na katika uhai wake alisomea Uhandisi na baadaye kujiendeleza katika fani za Sheria na Usimamizi wa Biashara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa