Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amelipokea kundi la viongozi, wakufunzi, maafisa na wanachuo kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) waliopo Mkoani Mara katika ziara ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa kozi ya 13 ya Chuo hicho na kuwataka wageni hao kuwa mabalozi wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika hafla ya mapokezi ya ugeni huo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji, Mhe. Mtambi amewataka viongozi, maafisa na wanachuo hao kuyatangaza mambo mazuri watakayoyaona katika Mkoa wa Mara na hususan katika sekta watazitembelea katika ziara hiyo.
“Mkoa wa Mara una mambo mengi mazuri na fursa nyingi za kiuchumi katika sekta za utalii, madini, kilimo, viwanda na biashara” na kuongeza kuwa “Mara ina kapeti la dhahabu, kuna migodi ya madini katika Wilaya zote sita za Mkoa wa Mara” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka wageni hao kuhakikisha wanapata nyama choma na kichuri ili kuonja radha tamu ya nyama za Mkoa wa Mara na kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kujionea uzuri wa hifadhi hiyo inayopatikana katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi amesema kundi lililopo katika Mkoa wa Mara litatembelea Wilaya za Butiama, Tarime, Musoma na Serengeti na litapita katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, kumbukumbu na historia, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mheshimiwa Mtambi amewataka wanachuo na wakufunzi hao kufanyia upembuzi masuala ya kiutamaduni, kisiasa, kijamii na kiuchumi na kutoa mapendekezo wakati wa kuhitimisha ziara hiyo ya mafunzo katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kutoa ushirikiano kwa kuwapokea na kuwapa msaada na taarifa zinazohitajika ambapo wanatarajiwa kuwepo kwa muda wa siku tano kuanzia leo tarehe 13 Januari, 2025 hadi tarehe 18 Januari, 2025.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Chuo Taifa cha Ulinzi (NDC) Meja Jenerali Balozi Wilbert Augustin Ibuge amesema Chuo hicho kinatoa mafunzo mbalimbali ya muda mrefu na mafunzo ya muda mfupi kulingana na mahitaji ya Taasisi mbalimbali wao.
Meja Jenerali Ibuge ameeleza kuwa katika mwaka wa masomo 2024/2025 Chuo hicho kina wanachuo 61 wa kundi la 13 ambao walianza mafunzo ya darasani Septemba, 2024 na wanatarajiwa kukamilisha mafunzo yao Julai, 2025 na kati yao wanachuo 41 wanatoka Tanzania na wanachuo 15 wanatoka katika mataifa rafiki.
Mhe. Ibuge amesema, jumla ya wanachuo wakiwemo watanzania 10 na wanafunzi kutoka nchi nyingine watano wamefika Mkoa wa Mara kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo na kueleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kujifunza kuhusu utekelezaji wa Sera za Taifa uwandani katika sekta mbalimbali.
Meja Jenerali Ibuge ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amesema katika awamu hii mikoa iliyotembelewa na makundi ya wanachuo hao ni pamoja na Mara, Kagera, Ruvuma. Mtwara, Katavi, Songwe, Pwani na Morogoro.
Chuo cha Taifa cha Ulinzi kilianzishwa rasmi mwaka 2011 na kilizinduliwa rasmi Septemba, 2012 na makao makuu yake yakiwa Jijini Dar es Salaam.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa