Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Afred Mtambi leo amekabidhi gari na pikipiki 15 ambazo zitatumika kwa ajili ya kusambaza chanjo katika Mkoa wa Mara na kuwataka wataalamu kuvitumia vifaa hivyo kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa hivyo, Mhe. Mtambi amesema gari na pikipiki hizo ni mpya na amezikagua zipo vizuri hivyo zikitumika vizuri kwa makusudi yaliyokusudiwa vinaweza kudumu na kutoa huduma kwa muda mrefu.
“Watumishi tutakaovitumia vifaa hivi tuhakikishe tunavitunza na kuvitumia kwa makusudio stahiki, nivikagua vyote na nimeendesha gari hili, vifaa hivi ni vipya kabisana ni vya viwango vya hali ya juu, twendendi tukavitumie kwa makusudio stahiki” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akitujali watanzania kwa kutoa vifaa hivyo kwa ajili ya kurahisisha zoezi la chanjo katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi amewataka wazazi kuwapeleka watoto kwenye chanjo na kuepuka imani potofu kuhusu baadhi ya chanjo zinazotolewa hapa nchini na kuwatahadharisha kuhusu umuhimu wa watoto kupata chanjo mapema ili kuweza kuwakinga na magonjwa mbalimbali.
Awali akitoa taarifa kuhusiana na vifaa hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya amesema gari na pikipiki hizo zimetolewa na Wizara ya Afya kwa ajili ya zoezi la chanjo katika Mkoa wa Mara.
Bwana Kusaya amesema gari hilo litatumiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa ajili ya kusambaza chanjo, wakati pikipiki 15 zimegawiwa kwenye Halmashauri zote kwa ajili ya matumizi ya wasimamizi wa chanjo na Halmashauri sita kati ya tisa zimepatiwa pikipiki mbili mbili.
Bwana Kusaya ameishukuru Wizara ya Afya kwa kutenga bajeti ya kuimarisha vitendea kazi kwa wataalamu wa afya na hususan vifaa hivyo ambavyo vimetolewa kwa ajili ya usimamizi wa zoezi la chanjo katika Mkoa wa Mara.
Gari la kusambaza chanjo limekabidhiwa kwa Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii wakati pikipiki zimekabidhiwa kwa Wakuu wa Wilaya kwa ajili ya kukabidhiwa Halmashauri mbalimbali zilizopo katika Mkoa wa Mara.
Hafla ya kukabidhi vitendea kazi hivyo imehudhuriwa Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Timu ya Usimamizi wa Sekta ya Afya Mkoa, Waganga Wakuu, Maafisa Lishe, Waweka Hazina, Maafisa Utumishi, Maafisa Elimu Msingi na Sekondari na Maafisa Mipango wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa