Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 15 Aprili, 2025 amezindua Kamati ya Maji Dakio la Mara na kuitaka kamati hiyo kutimiza wajibu wake katika kusimamia rasilimali za maji katika Mkoa wa Mara.
“Maji ni rasilimali muhimu sana duniani, ikitumiwa vibaya inaweza kusababisha vita kati ya nchi nan chi, jamii na jamii lakini bodi hii ikitimiza wajibu wake vizuri maji yatakuwepo kwa wingi. Kutokana na hilo, kazi mliyopewa ni kubwa sana ikifanywa vizuri inaleta amani” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka wajumbe walioteuliwa kwa mara ya pili kuongeza bidi na wajumbe wapya wa Kamati hiyo kuongeza ari katika utekelezaji wa majukumu yao ili waweze kuacha alama chanya katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi ameitaka Kamati hiyo kuanza kushughulikia changamoto mbalimbali zilizobainishwa na LVBWB katika hafla hiyo na kuomba msaada unaohitajika katika ngazi za Mkoa, Wilaya na Halmashauri ili kwa kushirikiana waweze kuzitatua changamoto hizo au kuzipunguza kwa kiasi kikubwa.
Mhe. Mtambi ameitaka Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi za Wilaya, Kata na Vijiji kuchukua hatua kali kwa wanaoingiza mifugo kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na kufuatilia taarifa za kuwepo kwa shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 za kingo za mto Rubana katika Wilaya ya Serengeti.
Mhe. Mtambi ameitaka pia Bodi hiyo kufuatilia na kubaini visima vyote vilivyochimbwa katika Mkoa na kutoa elimu kuhusu madhara ya kuchimba visima kiholela na kuhamasisha utunzaji wa vyanzo vya maji kwa wananchi.
Kanali Mtambi amesema jukumu la kutunza mabonde ya maji ni jukumu la wananchi wote kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinatunzwa kwa sababu yatakapokosekana maji, watakaopata shida ni watu wati wote.
Mhe. Mtambi amewataka wasimamizi wa mazingira kuhakikisha wananchi wanaopewa vibali vya kukata miti wawe wamepanda miti na kuendelea kutoa elimu kuhusiana na umuhimu wa kupanda miti inayotunza mazingira katika maeneo yao.
Aidha, amezitaka Halmashauri kuhamasisha wananchi kuhusu ufugaji wa kisasa na faida zake ili kusaidia katika utunzaji wa mazingira na kuanzisha utamaduni wa kuchukua hatua kwa haraka mtu anapokiuka utaratibu kwa kuwa wananchi wakiona hamna hatua za haraka zinazochukuliwa wanajua jambo hilo ni sahihi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria Dkt. Bonaventure Thobias Boya amesema usimamizi wa masuala ya maji hapa nchini unafuata mifumo ya kidunia ya Basin approach ambapo nchiya Tanzania imegawanywa katika mabonde tisa ya usimamizi wa rasilimali za maji na Bonde la Maji la Ziwa Victoria ni moja wapo.
Dkt. Boya amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla hii ya uzinduzi wa kamati ya Dakio la Mara na kuongeza kuwa kwa kuizindua Kamati hiyo rasmi inawapa nguvu wajumbe wa Kamati hiyo kutekeleza majukumu yao.
Dkt. Boya amewapongeza wajumbe wa Kamati ya Dakio la Mara kwa kuteuliwa na kukubali uteuzi huo na kuwataka kuhakikisha kuwa rasilimali za maji katika Bonde la Ziwa Victoria zinakuwa endelevu na kutekeleza majukumu yao wakiongozwa na kujitolea, uadilifu, kutokuchoka, uvumilivu.
Dkt. Boya amesema maji ni moja ya agenda muhimu za Kitaifa na ikisimamiwa vizuri inaleta amani na utulivu kwa wananchi na baina ya nchi na nchi.
Aidha, Mwenyekiti huyo amewashukuru wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Serikali walioshiriki katika hafla hiyo kama wadau muhimu wa maendeleo ya Sekta ya Maji.
Kwa upande wake, Mhandisi Mwita Mataro Afisa wa Maji Dakio la Maji la Bonde la Ziwa Victoria amesema Kamati ya Maji ya Dakio la Bonde la Mto Mara iliundwa rasmi Agosti, 2025 miaka mitatu.
Mhandisi Mataro amesema wajumbe wa Kamati ya Dakio la Mara wanapatikana kutokana na jukwaa la watumia maji wote wa Mkoa wa Mara ambao wanapendekeza majina ya watu kuwawakilisha kwenye Bodi ya Bonde la Ziwa Victoria na majina machache kuunda kamati.
Akitoa taarifa katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji wa Bonde la Ziwa Victoria Dkt. Renatus James Shinkuh amesema jukumu kubwa la LVBWB ni kuhakikisha rasilimali za maji za maji zinatunzwa na kuhifadhiwa.
Dkt. Shinkuh amesema majukumu makuu ya taasisi hiyo yawameweka katika makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutathmini na kufuatilia rasilimali za maji, kugawa maji kwa watumiaji mbalimbali, kulinda na kutunza rasilimali za maji.
Amesema wanazo maabara za kupima ubora wa maji zenye ithibati katika Miji ya Musoma, Mwanza na Bukoba na taarifa zinazotolewa na maabara hizo zinakidhi matakwa ya ubora kitaifa na kimataifa, vituo vya kupima wingi wa maji katika mito na ziwa na vituo vya kupima hali ya hewa katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Dkt. Sinkuh amesema Bodi hiyo inatoa vibali mbalimbali vya matumizi ya maji na kipaumbele katika ugawaji wa maji ni matumizi ya binadamu, mazingira na shughuli za kiuchumi na katika kutunza vyanzo vya maji bodi hiyo inaweka mipaka kuainisha maeneo ya vyanzo vya maji na kupanda miti rafiki ya maji.
Dkt. Sinkuh amezitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na wimbi kubwa la watu kuvamia vyanzo vya maji, ukataji wa miti katika maeneo yaliyohifadhiwa, kuingiza mifugo kwenye maeneo ya vyanzo vya maji, ushirikiano mdogo wa wananchi, uchimbaji holela wa visima vya maji.
Dkt. Sinkuh amesema taasisi yake inahudumia Mikoa mitano ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita na Simiyu na kuongeza kuwa maji ya ziwa Victoria yanatokana na mito kwa asilimia 20 na asiliami 80 ya maji yanatokana na mvua huku ziwa hilo likiwepo katika nchi za Tanzania, kenya na Uganda.
Tukio hilo limehudhuriwa viongozi na watendaji wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, wajumbe wa kamati iliyozinduliwa, wawakilishi wa taasisi za Maji za Mkoa wa Mara, baadhi ya watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa