Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi akiambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara ametembelea eneo lenye mgogoro wa ardhi katika mpaka wa Kata ya Mwema na Regicheri, Wilaya ya Tarime na kuwataka wananchi kujifunza kutatua changamoto zao kwa amani.
“Sio kila changamoto inahitaji utatuzi wa kutumia nguvu na mapanga, changamoto nyingine zinazungumzika kwa amani na utulivu na inapatikana suluhu ya kudumu” amesema Mhe. Mtambi na kuongeza kuwa “hapa hamna mshindi wala bingwa katika mgogoro huu”.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi kuhakikisha kuwa mgogoro huu unatatuliwa kwa amani na utulivu na kuwahakikishia wakiendelea na mgogoro huo atatoa kipande kinachogombewa kwa uongozi wa JKT ili wenyemashamba katika eneo hilo wafanye kazi chini ya uongozi wa kijeshi.
Mhe. Mtambi amemwagiza Kamishana Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mara kutambua mpaka wa Kata hizo na kuuangalia mpaka wa Inglam uliowekwa na Serikali ya Wakoloni sambamba na utambuzi wa wamiliki halali wa mashamba katika eneo linalogombewa.
“Baada ya kukamilisha utambuzi wa mipaka na wamiliki wenyemashamba katika eneo linalogombewa nitakuja kutoa maamuzi ya Serikali kuhusu mgogoro huu” amesema Mhe. Mtambi na kuwataka wananchi ambao hawana mashamba katika eneo hilo kuacha kuchochea mgogoro huo.
Mhe. Mtambi amemtaka Bwana Laurent Nyablanketi mfanyabiashara anayekodisha mashamba katika eneo hilo kuacha kuendelea kuchochea mgogoro huo na kuendelea kufanyabiashara zake katika eneo hilo kwa amani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele amesema baada ya kuibuka mgogoro kwa siku za hivi karibuni alitoa maelekezo ya wananchi kuacha kufanya maendelezo yoyote katika eneo lenye mgogoro hadi hapo mgogoro huo utakapotatuliwa.
“Hii ilitokana na baadhi ya sababu za kuibuka kwa mgogoro katika eneo hili kwa wakati huu ni baada ya baadhi ya wananchi kuanza kujenga nyumba katika eneo lenye mgogoro na hivyo kuendelea kuchochea mgogoro huo” amesema Mhe. Gowele.
Mhe. Gowele amesema katika eneo hilo kuna mashamba matatu yenye hati ambayo wananchi wanasema hawawatambui wamiliki wa mashamba hayo na wamiliki hao wamekuwa wakiyakodisha mashamba hayo pamoja na kuwa eneo hilo linamgogoro wa umiliki wa mashamba hayo.
Mhe. Gowele amewashukuru wazee wa mila wa koo zenye mgogoro katika eneo hilo kwa kusaidia kutuliza mgogoro wakati Serikali ikitafuta suluhisho la kudumu la mgogoro huo.
Mgogoro huo umedumu takribani miaka 30 ukiibuka na kutulia na unazihusisha koo za Wanchari na Wakira katika vijiji vya Remugwe na Kolotambi katika kata za Mwema na Regicheri, Tarafa ya Sirari, Wilaya ya Tarime.
Katika ziara hiyo, walishiriki pia Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, watumishi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na baadhi ya viongozi na maafisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa