Mkuu wa Mkoa wa Mara leo amezindua kampeni ya uhamasishaji wa chanjo ya mifugo inayotolewa kwa ruzuku ya Serikali na kuwataka wafugaji wa Mkoa wa Mara kuchangamkia fursa ya kampeni hiyo na kujitokeza kwa wingi kuchanja mifugo yao.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amesema Serikali imewekeza katika kuwasaidia wananchi kuweza kujiimarisha kiuchumi hata hivyo ni jukumu la mwananchi mmoja mmoja kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali katika kuboresha maisha na uchumi wao kupitia fursa hizo zilizopo katika sekta mbalimbali.
“Niwatake wafugaji wote wa Mkoa wa Mara kushiriki kampeni hii kwa kupokea elimu kutoka kwa wataalamu kuhusu chanjo za mifugo na kuchanja mifugo yote kwa bei ya ruzuku wakati huu Serikali inapotoa chanjo hizo” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya, viongozi wa Halmashauri na Wataalamu wa mifugo pamoja na wadau wa sekta ya mifugo kwenda kutoa elimu kwa wananchi na kuwahakikishia kuwa chanjo hizo ni salama na zote zimetengenezwa hapa nchini.
Mhe. Mtambi amewataka wataalamu na viongozi kusimamia utoaji wa chanjo hizo ili zisitoroshwe kwenda nje ya nchi na kuwaonya watu wote wanaojipanga kuzitorosha chanjo hizo kuwa Kamati ya Usalama ya Mkoa itakuwa makini kufuatilia utoaji wa chanjo hizo katika Mkoa wa Mara.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka wataalamu wa mifugo kuona namna ya kuwabainisha wafugaji wa Tanzania nan chi jirani ili ruzuku iliyotolewa na Serikali iwanufaishe wafugaji wa Tanzania ambao ndio walengwa wa kampeni hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Bwana Mrida Mshota akizungumza katika kikao hicho amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa ruzuku ya chanjo ya mifugo kwa wafugaji hapa nchini.
“Hii ni mara ya kwanza kwa nchi yetu kuwasaidia wafugaji kwa kuwapa chanjo za ruzuku, kwa niaba ya wafugaji wote tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuwafikia wafugaji” amesema Bwana Mshota.
Bwana Mshota amesema Serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya wafugaji ikiwemo kujenga shule, zahanati, malambo na majosho ya mifugo kwenye maeneo ya wafugaji ambayo awali hayakuwa na miundombinu hiyo.
Bwana Mshota amewaomba Wakuu wa Wilaya, viongozi wa Halmashauri na wataalamu wa mifugo kwa kushirikiana na vyama vya wafugaji kuwahamasisha wafugaji kushiriki katika kampeni ya utoaji wa chanjo hiyo ya ruzuku na kuwafafanulia wafugaji kuhusu madhara ya wao kutokuchanja mifugo yao.
Aidha, Bwana Mshota amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Mtambi kwa kazi nzuri anayoifanya katika Mkoa wa Mara na kuahidi kumpatia ng’ombe mmoja wa maziwa kutambua uongozi wake unavyowasaidia wananchi wa Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Tawala Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Bwana Musiba Mingistus Nandiga ameeleza kuwa Mkoa wa Mara una ng’ombe 4,745,411 na kati ya mifugo hiyo ng’ombe ni 1,451,484, mbuzi 707,442, kondoo 569,536, kuku 1,742,557 na wanyama wengine.
Bwana Nandiga amesema kampeni ya chanjo itahusisha utoaji wa chanjo kwa ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku ambapo magonjwa yatakayopatiwa chanjo ni pamoja na ugonjwa wa homa ya mapafu kwa ng’ombe, sotoka kwa mbuzi na kondoo na mdondo kwa kuku.
“Uhamasishaji wa wananchi kwa ajili ya kampeni hii utafanyika kuanzia leo tarehe 22 Januari, 2025 hadi tarehe 9 Februari, 2025 na uhamasishaji utafanywa na viongozi na wataalamu wa sekta ya mifugo” amesema Bwana Nandiga.
Bwana Nandiga amesema kuwa chanjo hiyo itatolewa kwa awamu ambapo ng’ombe, mbuzi na kondoo watapatiwa chanjo kuanzia tarehe moja Februari, hadi tarehe 30 Machi, 2025 wakati kuku watachanjwa tarehe moja Mei, 2025 hadi tarehe 30 Mei, 2025.
Bwana Nandiga amesema katika kampeni hiyo wananchi watatakiwa kuchangia fedha kidogo katika uchanjaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo hata hivyo chanjo ya kuku itatolewa bure kwa wananchi wote.
Bwana Nandiga amesema wajibu wa wananchi ni pamoja na kujitokeza na kushiriki katika kampeni hiyo ili mifugo yao iweze kupatiwa chanjo ya kuzuia mlipuko wa magonjwa hayo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa, wataalamu kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, viongozi wa Dini, Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Halmashauri, wadau wa kilimo, mifugo na biashara katika Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa