Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo ametembelea ujenzi wa Barabara ya Mogabiri- Nyamongo (Km 25) inayojengwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kuwataka wakandarasi wazawa kujiongeza kwa kuboresha utendaji wao ili waweze kushindana katika zabuni za kimataifa.
Mhe. Mtambi amesema wakandarasi wazawa wanauwezo mkubwa wa kufanyakazi mbalimbali na hata kugombea zabuni za kimataifa kama watakuwa makini katika utendaji wao wanapotekeleza miradi wanayopewa.
“Mkiacha tabia ya kukimbilia kuongeza wake na kufanya starehe baada ya kupata malipo ya kutekeleza miradi vizuri mtafanikiwa na mtafika mbali katika kushindania zabuni na kutekeleza miradi” amesema Mhe. Mtambi.
Akizungumzia kuhusu barabara hiyo, Mhe. Mtambi amesema amekagua na kuridhishwa na kazi inayoendelea katika utekelezaji wa mradi huo na kumtaka mkandarasi kukamilisha barabara hiyo kwa mujibu wa mkataba.
“Hii ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa Mkoa wa Mara na inaunganisha Wilaya za Tarime na Serengeti na inawaunganisha watalii wanaopitia nchi ya Kenya kuingia katika Hifadhi ya Serengeti kiurahisi zaidi” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, amesema barabara hiyo ni muhimu kwa kusafirisha mazao ya kilimo na wananchi kiurahisi kwenda katika maeneo mbalimbali na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Mara kumshukuru Mhe. Rais kwa kufanikisha mradi huo na kusaidia katika kuutunza ili udumu muda mrefu.
Mhe. Mtambi amesema kuna baadhi ya Wilaya ambazo makao makuu yake hayajaunganishwa na lami katika Mkoa wa Mara lakini Mhe. Rais baada ya kuliona hilo ameanzisha miradi mbalimbali ambayo itasaidia kuondoa tatizo hilo.
Wakati huo huo, Mhe. Mtambi amekemea wazabuni na wakandarasi waliopewa zabuni na wanaokwamisha utekelezaji wa miradi katika Mkoa wa Mara na kuwatahadharisha kuwa Mkoa utachukua hatua stahiki kuhakikisha hawapati tena zabuni katika Mkoa wa Mara.
“Kama mzabuni au mkandarasi unajiona huna uwezo wa kuleta vifaa na kutekeleza mradi usiombe zabuni katika Mkoa wa Mara, tutakuchukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwablacklist wasifanye kazi katika Mkoa wa Mara” amesema Mhe. Mtambi.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara Mhandisi Vedastus Maribe amesema utekelezaji wa barabara hiyo upo katika nzuri na tayari mkandarasi ameshajenga madaraja makubwa saba na madaraja madogo zaidi ya 30 na barabara yenye urefu wa kilometa sita imekamilika na imeanza kutumika.
“Utekelezaji wa mradi huu upo katika asilimia 56 na unatarajiwa kukamilika mwaka huu kwa mujibu wa mkataba” amesema Mhandisi Maribe.
Akizungumzia kuhusu barabara nyingine zinazoendelea kujengwa katika Mkoa wa Mara, Mhandisi Maribe amesema kwa sasa kuna miradi ya barabara mitatu ya barabara za kuelekea Mji wa Mugumu inayoendelea kujengwa ikiwa katika hatua mbalimbali.
Mhandisi Maribe amesema ujenzi wa barabara za Musoma- Busekela katika eneo la Kusenyi- Musoma (km 40) na barabara ya Utegi -Shirati (km 27) upo katika hatua za zabuni ya kuwapata wakandarasi.
Kwa upande wake, Mama Monica Charles Josia Mkazi wa Kijiji cha Komerele amemshukuru Mhe. Rais kwa kujenga barabara hiyo na kuongeza kuwa imewaondolea adha ya usafiri na kwa sasa wanapata usafiri kwa bei nafuu.
“Zamani tulikuwa tunaenda Tarime Mjini kwa shilingi 10,000 na kurudi inakuwa shilingi 20,000 lakini sasa nauli imekuwa ni shilingi 2,000 tu kwenda na kurudi inakuwa 4,000; hatukuwahi kulipa nauli ndogo kiasi hiki” amesema Mama Josia.
Mama Josia amemshukuru pia Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mhe. Mwita Waitara kwa ufuatiliaji wake wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika jimbo hilo na Mkoa wa Mara kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa