Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe ngazi ya Mkoa kwa kipindi cha Julai- Desemba kwa mwaka 2024/2025 na kuzitaka Halmashauri kuongeza uhamasishaji katika masuala ya uchangiaji wa chakula ili wanafunzi wote wa Mkoa wa Mara waweze kupata chakula shuleni.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amesema Halmashauri hazijafanya uhamasishaji wa kutosha kuhusu uchangiaji wa chakula kwa hiari na haziwatumiaa wadau mbalimbali waliomo katika Halmashauri zao wakiwemo viongozi wa dini, viongozi wa kimila na mashirika yasiyo ya kiserikali.
“Tangu nimekuja Mkoa wa Mara nimeona mkutano mkubwa mmoja tu kuhusiana na masuala ya ulishaji chakula shuleni na ambao uliandaliwa na ofisi yangu, lakini Halmashauri sijaona inafanya jambo kubwa kuhusiana na uhamasishaji wa kuchangia chakula shuleni” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema wakati wa kikao cha tathmini ya kitaifa Agosti, 2024 Mkoa wa Mara ulikuwa ni miungoni mwa mikoa 11 iliyofanya vibaya ya utoaji wa chakula mashuleni jambo ambalo halikubaliki wakati Mkoa wa Mara ndio ulikuwa wakwanza kufanyiwa majaribio na mwongozo wa Kitaifa wa utoaji wa chakula shuleni umetayarishwa Mara.
“Mimi niliambiwa mikoa ambayo awali ilikuja kujifunza Mara kutoa chakula shuleni inafanya vizuri kuliko Mkoa wa Mara ambao ulikuwa wakwanza kitaifa na ulishiriki kuandaa mwongozo wa utoaji wa chakula kwa wanafunzi, hilo halikubaliki, tubadilike” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amezitaka Halmashauri zote kutunga sheria ndogo ndogo za kuwabana wazazi na walezi wa wanafunzi kuchangia chakula mashuleni ili wasipochangia kwa hiari wabanwe kuchangia ili watoto wapate chakula wakiwa shuleni.
Mhe. Mtambi amewataka viongozi, wasimamizi wa elimu na watendaji kwa ujumla kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chakula angalau mara moja shuleni na kuhakikisha uchangiaji kwa kupitia wazazi, walezi na wadau unafanyika.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Mkoa wa Mara Bibi Grace Martin amesema shule nyingi zinatoa huduma ya chakula shuleni hata hivyo idadi ya wanafunzi wanaopata shuleni bado ipo kidogo kwa sababu sio watoto wote wanaopata chakula shuleni.
Bibi Martin amesema kutokana na uchangiaji wa wazazi na walezi na sababu nyingine shule nyingi zinatoa huduma za chakula kwa wananfunzi wachache jambo ambalo ni kinyume na miongozo ya Serikali kuhusu utoaji wa chakula shuleni.
Bibi Martin amesema kwa sasa Mkoa wa Mara una wastani wa asilimia 68 ya utoaji wa chakula shuleni na Halmashauri ya Tarime TC imefanya vizuri katika uchangiaji wa chakula shuleni.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bwana Gerald Kusaya, Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya, Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Timu ya Usimamizi wa Sekta ya Afya Mkoa, Waganga Wakuu, Maafisa Lishe, Waweka Hazina, Maafisa Utumishi, Maafisa Elimu Msingi na Sekondari na Maafisa Mipango wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa