Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameshiriki kikao Maalum cha Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuitaka Halmashauri hiyo kuanzisha Serengeti Tourism Fair.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Mtambi ameitaka Wilaya kuanza kujipanga kwa ajili ya kuanzisa maonesho ya Serengeti Tourism Fair katika msimu ujao wa kitalii.
“Tuanze mwakani na tuone namna ya kufanya Serengeti Toursim Fair kila mwaka hapa Serengeti na kushirikisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kushiriki na kufadhili maonesho hayo” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema Mkoa kwa sasa unalengo la kuzitangaza fursa mbalimbali za uwekezaji ili kuwakaribisha wawekezaji zaidi kuwekeza katika Mkoa wa Mara katika fursa mbalimbali zilizopo katika Mkoa.
Mhe. Mtambi pia ameitaka Halmashauri hiyo kufanya upembuzi yakinifu wa kubaini haki na stahiki za Halmashauri katika uwekezaji uliofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) ili kuboresha mapato ya Halmashauri hiyo.
Mhe. Mtambi amelitaka Baraza la Madiwani kushirikiana na Menejimenti ya Halmashauri hiyo kuboresha makusanyo katika vyanzo vya mapato vilivyopo na kuongeza vyanzo vya mapato vipya ili kuiwezesha Halmashauri hiyo kujiendesha na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Mhe. Mtambi ameitaka Halmashauri kufanya upembuzi wa kina kuhusiana mapato ya Halmashauri yanayotokana na shughuli za uchimbaji madini ndani ya Halmashauri hiyo ya Serengeti.
Mhe. Mtambi amewataka wataalamu wa Halmashauri kutoa elimu kwa vikundi vya wanawake, vijana, watu wenye ulemavu wanaopewa mikopo ya Halmashauri ili waweze kuendelea na kunufaika na mikopo hiyo ili wananchi wajenge hulka ya kukopa na kuwa na nidhamu ya fedha.
Mhe. Mtambi ameahidi kuendelea kufuatilia Serikalini suala la makampuni yanayofanya shughuli zake ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kulipa ushuru wa huduma nje ya Halmashauri hiyo wakati shughuli zao zikifanyika Serengeti.
Mhe. Mtambi amesema Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ina barabara mbovu ukilinganisha na Wilaya nyingine na Mkoa unajitahidi kujenga hoja ili barabara za Serengeti zitengenezwe kwa haraka kuwavutia watalii na wananchi wapate unafuu katika usafiri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mhe. Kemilembe Lwota ameshukuru Halmashauri hiyo kwa kuongeza jitihada katika ukusanyaji wa mapato ambapo amesema kwa sasa Halmashauri hiyo imekusanya kwa asilimia 107 ya bajeti iliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mhe. Lwota ameumshukuru uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa miongozo na maelekezo wanaoupata na kulipongeza Baraza la Madiwani, Mkurugenzi, Menejimenti na watumishi wote wa Wilaya hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mhe. Lwota amesema makusanyo ya mapato yakiendelea kama ilivyo sasa, Wilaya ya Serengeti inaenda kuwa ya viwango vingine tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mhe. Ayub Mwita Makuruma amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi kwa kazi kubwa anayoifanya katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa sasa Halmashauri hiyo inaendelea vizuri na kero nyingi zimetatuliwa na wananchi wanaendelea na shughuli zao.
Mhe. Makuruma amesema Halmashauri hiyo ina hoja chache, kwa mwaka 2023/2024 Halmashauri ina hoja mpya nane na zote zinatekelezeka lakini kuna baadhi ya hoja za zamani hazitekelezeki kwa sasa kutokana na aina ya hoja zilizopo.
“Mfano wa hoja ambazo hazitekelezeki, ni hoja kuhusiana na kutokupeleka fedha za miradi ya maendeleo kutokana na hali mbaya kimapato iliyokuwepo katika mwaka wa 2020-2021 na ilivyoathiri mapato ya Halmashauri kutokana na tatizo la Covid 19” amesema Mhe. Makuruma.
Mhe. Makuruma amesema katika kipindi hicho Halmashauri ilikuwa katika hali mbaya kimapato ambapo ilifanikiwa kukusanya asilimia 51 tu ya mapato kwa mwaka huo kutokana na kupungua kwa watalii na kulihakikishia baraza kwa sasa Halmashauri hiyo inafanya vizuri katika makusanyo.
Mhe. Makuruma amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri Bajeti imepanda 4.7 kwa sasa wapo 5.5 asilimia 107 ya makusanyo na kuongeza kuwa katika bajeti ya 2025/2026 Halmashauri hiyo imejipanga kukusanya zaidi ya shilingi bilioni sita.
Mhe. Makuruma amesema kwa sasa Halmashauri hiyo haikusanyi vizuri katika vyanzo vilivyopo katika Hifadhi ya Serengeti baadhi ya makampuni yameanza kulipa ushuru wa huduma katika Halmashauri ya Seregeti hata hivyo bado kuna makampuni sita ambayo bado yanaleta shida na mazungumzo yanaendelea.
Amemuomba Mkuu wa Mkoa kuisaidia Halmashauri hiyo katika kutatua kero hiyo ili Halmashauri iweze kukusanya fedha vizuri za kuweza kujiendesha na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa faida ya wananchi wa Halmashauri hiyo.
Akiwasilisha hoja za ukaguzi, Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Bibi Veronica Lukanda amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ilipata hoja 49 na baada ya uhakiki hoja 22 zilijibiwa na kufungwa, hoja tatu zimejirudia na hoja 24 zimebakia.
Bibi Lukanda amesema Halmashauri ilipata hoja 23 katika Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund) na kati yake hoja 15 zimefungwa na hoja nane zinaendelea kutekelezwa na katika Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu Halmashauri ilipata nne na kati yake hoja moja ilijirudia, hoja tatu zinaendelea kutekelezwa.
Bibi Lukanda amesema katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) cha tarehe 08 Septemba, 2022, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ilipewa maagizo sita ambapo agizo moja limetekelezwa na kufungwa wakati maagizo matano utekelezaji wake unaendelea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Dkt. Maulid Madeni amesema wakati amehamishiwa katika Halmashauri hiyo aliikuta ikiwa na changamoto kubwa tatu ambazo ni mapato ya Halmashauri, hoja za ukaguzi za miaka ya nyuma na uharibifu mkubwa wa barabara kutokana na ufinyu wa bajeti ikilinganishwa na ukubwa wa Halmashauri.
Dkt. Madeni amesema kwa sasa imeibuka changamoto nyingine ya uchafu wa Mji wa Mugumu unaotokana na wazabuni wanaoshinda zabuni za ukandarasi wa kuzoa taka kufanyakazi kutokuwa makini katika shughuli zao na kuvunja mkataba yao.
Dkt. Madeni amesema katika kutatua changamoto hizi, Halmashauri inahitaji makusanyo na hususan kutoka katika chanzo cha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti walifanikiwa kuonana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na kwa sasa baadhi ya kampuni zimeanza kulipa ushuru wa huduma katika Halmashauri hiyo.
Kikao hicho kilihudhuliwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti, baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Ofisi ya Ukaguzi, Madiwani, Mkurugenzi na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa