Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameshiriki Baraza Maalum la Madiwani kuhusu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na kuipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi kwa mfululizo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amesema hati safi zilizopatikana zinaonyesha jitihada kubwa ambayo Baraza la Madiwani, Menejimenti na Watumishi wameifanya katika kusimamia mapato na matumizi ya Halmashauri hiyo.
“Kwa kupata hati safi kwa mfululizo inaonyesha kuwa mnafanya vizuri na wakaguzi hawana mashaka na utendaji wenu, hongereni sana” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ameitaka Halmashauri hiyo kupunguza hoja za ukaguzi kwa kufuta baadhi ya hoja ambazo majibu yake wanayo na kumtaka Mkurugenzi kuanzisha na kama kipo kukiimarisha Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini ili kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Kanali Mtambi ametaka Halmashauri hiyo kupeleka fedha za maendeleo ya vijiji kulingana na miongozo ya Serikali ya kutoa shilingi 200,000 kwa kila kijiji katika kipindi cha robo mwaka kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za vijiji.
Aidha, ameitaka Menejimenti kutekeleza kwa uadilifu majukumu yote ya Halmshauri katika kipindi ambacho kutakuwa hamna Baraza la Madiwani wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kuwatakia madiwani wote ushindi katika uchaguzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka amesema Wilaya itasimamia Halamshauri hiyo iweze kupunguza hoja za ukaguzi na wataiweka ajenda ya hoja ya ukaguzi katika vikao vyote vya Kamati ya Usalama ya Wilaya.
Mhe. Chikoka amesema viongozi wa Wilaya watazunguka katika vijiji kuhamasisha vijana kuweza kuchangamkia fursa ya mikopo ya Halmashauri na kuahidi kuwa watahakikisha vijana wengi wanatumia fursa hiyo kujishughulisha katika uzalishajimali na kuboresha maisha yao.
Akitoa taarifa katika Baraza hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Ndugu Msongela Palela amesema Halmashauri hiyo katika ukaguzi wa mwaka 2023/2024 imepata hati safi ya ukaguzi.
Amesema pamoja na kupata hati safi, Halmashauri ilikuwa na hoja 81 za ukaguzi pamoja na maagizo matano ya kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambapo hoja za nyuma zilikuwa 55 na hoja mpya zilikuwa 26.
Bwana Msongela amesema baada ya uhakiki Halmashauri ilibakia na hoja 69 pamoja na maagizo matano ya LAAC ambapo hoja za nyuma zilikuwa 49 na hoja mpya zilikuwa 20 na kati ya hoja zote zilizotekelezwa 20, zilizopitwa na wakati 2, nne zimehuishwa katika ukaguzi mpya, zinazoendelea kutekelezwa 21 ambazo bado kutekelezwa ni hoja 2.
Baraza Maalum la Madiwani limehudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, wajumbe wa Kamati ya Usalama wa Wilaya ya Musoma, baadhi ya watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, maafisa kutoka ofisi ya CAG, Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa