Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 17 Aprili, 2025 amepokea msaada kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na wazabuni wake kwa ajili ya waathirika waliokumbwa na maafa katika kata 10 za Manispaa ya Musoma na kuahidi kuwa Mkoa utasimamia misaada hiyo iweze kuwafikia walengwa waliokusudiwa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Mtambi ameushukuru mgodi kwa kutoa shilingi 45, 240,000, mifuko 200 ya simenti na magodoro 20 na kuwahakikishia kuwa msaada huo utatumika kulingana na malengo yaliyokusudiwa.
“Msaada huu umefika wakati muafaka ambapo tunaendelea kurejesha hali ya wananchi walioathirika katika maafa hayo kuwa nzuri zaidi kuliko hali waliokuwa nayo awali kabla ya maafa hayo” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema kwa sasa baadhi ya wahanga wa maafa hao wamesaidiwa kuanza kuishi maisha yao ya kawaida katika maeneo waliyotoka na wale waliokuwa wapangaji wamesaidiwa kwa kulipiwa kodi ya miezi sita kulingana na kodi zao za awali.
“Baada ya msaada uliotolewa na Rais Samia, waathirika wengi wamerejea katika hali zao za awali, aidha familia tatu ambazo nyumba zao ziliathirika zaidi zimejengewa nyumba mpya na kupatiwa majiko yanayotumia nishati safi ya kupikia” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema bado kuna watu wanaohitaji msaada ikiwemo ukarabati mkubwa wa nyumba zao ili waweze kurejea katika hali yao ya awali na ikiwezekana wapate hali bora zaidi.
Mhe. Mtambi ametumia fursa hiyo kuzipongeza Kamati ya Usalama na Kamati ya Maafa Mkoa na Wilaya ya Musoma kwa kazi nzuri walizofanya katika utekelezaji wa zoezi la kuwahudumia wahanga wa maafa hayo na kufanikisha kurejesha hali zao za awali kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka amesema katika maafa hayo jumla ya kata 10 ziliathirika na kaya 319 zenye watu 1,227 ziliathirika na maafa hayo ikiwa ni pamoja na majengo ya taasisi za Serikali, biashara na dini.
Mhe. Chikoka ameushukuru Mgodi wa North Mara kwa kusaidia jitihada za Serikali za kuwarejesha wahanga wa maafa hayo katika hali nzuri ili waendelee kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa upande wake Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu North Mara Bwana Francis Uhadi amesema Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kushirikiana na wazabuni mbalimbali waliopo mgodini hapo umetoa msaada wa fedha taslimu na vifaa.
Bwana Uhadi amesema Mgodi unatoa msaada wa fedha tasilimu shilingi 45,240,000 na tani kumi za simenti na magodoro 20 kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa maafa hayo.
Bwana Uhadi amesema Mgodi unatoa pole nyingi kwa wote waliofikwa na maafa hayo pamoja na viongozi na watumishi wa Serikali ambao walishiriki kwa namna moja au nyingine kutoa msaada wa kibinadamu kwa waathirika hao.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa