Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 23 Aprili, 2025 ameshiriki ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika ikiwa ni sehemu ya sherehe za miaka 61 ya Muungano katika Mkoa wa Mara ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati Katibu Mkuu wa CCM alipokuwa anakagua miradi ya Uwanja wa Ndege Musoma na Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa).
“Mhe. Rais amekuwa akiutazama Mkoa wa Mara kwa namna ya kipekee sana na amekuwa akileta fedha za kutekeleza miradi mingi ya kimkakati ambayo itachechemua maendeleo ya Mkoa na Nchi ya Tanzania” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeleta fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati katika sekta zote na imebadilisha mwelekeo wa maendeleo ya Mkoa kwa kiasi kikubwa sana.
Mhe. Mtambi amewaomba wananchi wa Mkoa wa Mara kumshukuru Rais na Serikali kali yake kwa vitendo na hususan kwa kuiunga mkono juhudi Serikali katika kuwaletea maendeleo na kuwakumbuka msemo kuwa “akufaae kwa dhiki ndio rafiki wa kweli”.
Mhe. Mtambi ametolea mfano Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya kwanza ya Serikali katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na inahudumia wagonjwa kutoka Mkoa wa Mara, Mikoa jirani na nchi jirani.
“Hili jengo ni kubwa sana japokuwa ujenzi wake ulianza zamani lakini jengo hili linauwezo wa helikopta kutua juu yake na mgonjwa kupokelewa hapa hapa hospitalini” amesema Mhe. Mtambi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma Mhe. Vedastus Mathayo amesema wananchi wa Mkoa wa Mara wameufuatilia ujenzi wa uwanja wa Ndege Musoma kwa muda mrefu na sasa unaenda kuanza kutoa huduma kuanzia Septemba, 2025.
Mhe. Mathayo amemuomba Mhe. Nchimbi kufuatilia fidia ya zaidi ya shilingi bilioni 5.2 wanaodai wananchi watakaopisha mradi wa ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja huo madai ambayo yametoka kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwenda Hazina kwa ajili ya malipo.
Mhe. Mathayo ameipongeza Serikali kwa miradi mingi inayoendelea kutekelezwa katika Wilaya ya Musoma ambayo amesema imebadilisha utoaji wa huduma kwa wananchi wa Manispaa ya Musoma na maeneo ya jirani.
Baada ya hapo, Ziara ya Mhe. Nchimbi iliendelea ofisi za Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara ambapo amekagua mradi wa ukumbi na kufanya kikao na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa iliyoboreshwa.
Kesho ziara ya Katibu Mkuu wa CCM inaendelea katika Wilaya ya Butiama ambapo anatarajia kutembelea Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJUNUAT) Butiama, kaburi la Baba wa Taifa na kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Kiabakari.
Katika ziara hiyo, Mhe. Nchimbi ameambatana na viongozi na Watendaji wa CCM na Serikali na kauli mbiu ya miaka 61 ya Muungano ni “Muungano wetu ni Dhamana, heshima na tunu ya Taifa, Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa