Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi leo anaanza ziara ya siku tano katika Mkoa wa Mara katika maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara inasema leo Mhe. Nchimbi anatarajiwa kupokelewa katika Wilaya ya Bunda mchana na baadaye kusalimia wananchi wa Wilaya ya Bunda katika eneo la Stendi ya Zamani, kabla ya kuendelea na safari ya kwenda Musoma.
Kesho tarehe 23 Aprili, 2025 ziara itaendelea katika Manispaa ya Musoma ambapo atakagua maendeleo ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma na baadaye kukagua maendeleo ya ujenzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuzungumza na wananchi katika eneo hilo.
Aidha, Mhe. Dkt. Nchimbi atatembelea Ofisi za CCM Mkoa wa Mara na kukagua ukumbi wa mikutano wa CCM unaoendelea kujengwa katika eneo hilo na baadaye atafanya kikao cha ndani na Halmashauri Kuu iliyoboreshwa.
Tarehe 24 Aprili, 2025 Mhe. Nchimbi atatembelea Kampasi ya Oswald Mwang’ombe na kukagua ujenzi wa Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia Butiama (MJUNUAT) na kutazuru kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na baadaye kuwasalimia wananchi wa Butiama katika eneo la Kiabakari.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa tarehe 25 Aprili, 2025 Balozi Nchimbi atafanya mkutano wa hadhara katika Mji wa Shirati katika Wilaya ya Rorya na baadaye atakagua ujenzi wa soko la kimkakati katika Mji wa Tarime na kufanya mkutano wa hadhara katika Mji wa Tarime.
Kwa tarehe 26 Aprili, 2025 Mhe. Nchimbi atakagua mradi wa maji Tarime- Rorya, atasalimia wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime njiani akielekea Serengeti, atafanya kikao cha ndani na kuhitimisha ziara hiyo kwa kufanya mkutano wa hadhara katika Mji wa Mugumu.
Katika ziara hiyo, Mhe. Nchimbi ataambatana na viongozi na Watendaji wa CCM na Serikali.
Kauli mbiu ya miaka 61 ya Muungano ni “Muungano wetu ni Dhamana, heshima na tunu ya Taifa, Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa