Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi leo ameendelea na ziara yake katika Wilaya ya Butiama ambapo ametembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kupewa kifimbo cha uongozi na familia ya Baba wa Taifa.
Mhe. Nchimbi akiwa katika eneo hilo amepokelewa na kiongozi wa kabila la Wazanaki Chifu Josephat Wanzagi na mtoto wa Mwalimu Nyerere Ndugu Madaraka Nyerere na wanafamilia wengine.
Dkt. Nchimbi ameishukuru familia ya Baba wa Taifa kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na akashukuru kwa zawadi ya fimbo na kuwaahidi kuyaenzi mazuri yote ambayo Baba wa Taifa aliyasimamia katika uhai wake.
Akizungumza wakati wa kukabidhi fimbo hiyo, Chifu Wanzagi amesema kifimbo hicho ni moja ya kifaa cha kazi atakachokitumia katika dhamana aliyopewa ya kuwatumikia Watanzania. na kuwataka watanzania kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo.
“Fimbo hii huwa tunamkabidhi kiongozi tunayemkubali, tunayeona anafaa kuwatumikia Watanzania na kwa kuwa tumeona unazo sifa hizo ndio maana tumekukabidhi” amesema Chifu Wanzagi.
Akiwa Mwitongo, Dkt. Nchimbi ametembelea kaburi la Baba wa Taifa na kuweka shada, kuwasha mshumaa, kufanya sala fupi katika kaburi hilo na kufanya mazungumzo na familia ya Mwalimu Nyerere.
Balozi Nchimbi ameambatana na Mwenza wake, Mama Jane Nchimbi pamoja na viongozi wengine wa Chama na Serikali ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Kauli mbiu ya miaka 61 ya Muungano ni “Muungano wetu ni Dhamana, heshima na tunu ya Taifa, Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa