Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo tarehe 22 Mei, 2025 amekabidhi magari mapya yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye thamani ya shilingi milioni 504 kwa ajili ya Wakuu wa Wilaya za Tarime na Musoma.
Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo kwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka na Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowelle, Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya kutumia magari hayo kutatua kero za wananchi katika maeneo yao.
“Tumieni magari haya kuwatembelea wananchi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kwa sasa hamna kisingizio cha kushindwa kufika sehemu yoyote kwa kuwa haya magari yanapita mahari popote hata ambapo hamna barabara nzuri haya yanapita” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema baada ya Mhe. Rais kutoa magari hayo amemaliza changamoto ya usafiri kwa Wakuu wa Wilaya ambapo awali magari kwa baadhi ya Wakuu wa Wilaya yalikuwa yanazimwa kutoka katika taasisi nyingine za umma lakini kwa sasa Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Mara wanayo magari mapya waliyonunuliwa na Mhe. Rais.
Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya kuyatunza magari hayo na kuhakikisha wanasimamia madereva wanayoyaendesha magari hayo ili waweze kuchukua tahadhari katika uendeshaji wao na kufuatilia ratiba za matengenezo ya kawaida ya magari hayo.
Kanali Mtambi ametumia fursa hiyo na kuwataka Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara kutumia magari hayo kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ili waweze kuchagua viongozi bora wanaopenda maendeleo.
Akizungumza katika hafla ya mapokezi ya gari hizo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowelle ameishukuru Serikali kwa kupatiwa magari ambayo yatawawezesha kufika katika maeneo yao ya utawala kwa haraka na kuwahudumia wananchi.
“Haya magari yatatusaidia sana kuwafikia wananchi na kusikiliza na kutatua kero zao, kukagua miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika Wilaya zetu na yataongeza kasi yetu katika kuwahudumia wananchi” amesema Mhe. Gowelle.
Mhe. Gowelle ameahidi kuwa watayatumia magari hayo kama yalivyokusudiwa na watasimamia kuhakikisha yanatunzwa na kutumika kwa shughuli za Serikali katika kuwahudumia wananchi na kuahidi kuyatunza ili yaweze kudumu muda mrefu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka watatekeleza maagizo yote ya Mkuu wa Mkoa na kuhakikisha magari hayo yanaleta tija kwa wananchi.
“Tunashukuru sana kwa kupatiwa magari haya ambayo yatatusaidia kufuatilia utekelezaji wa miradi na kutatua kusikiliza kero za wananchi kwa wakati” amesema Mhe. Chikoka.
Hafla ya kukabidhi magari hayo imehudhuliwa na Wakuu wa Wilaya, watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya na baadhi ya watumishi kutoka Ofisi za Wakuu wa Wilaya waliopokea magari hayo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa