Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 8 Julai, 2025 amepokea taarifa mbalimbali za Sehemu ya Elimu na kuwapongeza wanafunzi 2,891 wa Mkoa wa Mara waliopata ufaulu wa daraja la kwanza katika matokeo ya mtihani wa Kitaifa wa kidato cha sita yaliyotangazwa tarehe 7 Julai, 2025.
Mhe. Mtambi ametoa pongezi hizo baada ya kuarifiwa kuwa jumla ya wanafunzi 2,891 ambao ni sawa na asilimia 61.4 ya wanafunzi wote 4,708 wa Mkoa wa Mara waliofanya mtihani wa kidato cha sita wamefaulu na kupata daraja la kwanza.
“Ninapongeza sana kwa matokeo haya, shule zimejitahidi sana kuwasimamia wanafunzi vizuri na wanafunzi wote wamefaulu vizuri, hongereni sana” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ameitaka Sehemu ya Elimu kuandaa kikao cha tathmini ambacho kitatumika pia kuzipongeza shule, walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani huo hata hivyo amesema zawadi ya gari haitatolewa kwa kuwa hamna shule iliyoingia katika 10 bora za kitaifa.
“Kwa sasa Mkoa utatoa zawadi za kawaida hadi hapo shule zitakapofanya vizuri zaidi Mkoa utatoa zawadi ya gari kwa shule zitakazoingia kwenye 10 bora za kitaifa na hili linawezekana” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, Mhe. amewapongeza walimu na wanafunzi waliohusika na mtihani huo kwa kupata matokeo mazuri ambapo wanafaunzi waliopata daraja la pili ni 1,597 ambayo ni sawa na asilimia 33.9 na waliopata daraja la tatu ni 220 ambao ni sawa na asilimia 4.67 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Mwalimu Makwasa Bulenga amesema kuwa Mkoa wa Mara ulikuwa na jumla wanafunzi 4,708 waliofanya mtihani huo kutoka Shule za Sekondari 29 na wote wamepata ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu pekee.
Bwana Bulenga amesema shule iliyoongoza kwa ufaulu ni Shule ya Sekondari ya Bunda (Bunda) ambayo imeshika nafasi ya 25 kitaifa na nafasi ya saba kwa shule za Serikali kitaifa na kufuatiwa na Shule ya Sekondari Mkono (Butiama) na Shule ya Sekondari ya Tarime (Tarime).
Bwana Bulenga amesema katika Shule za Sekondari za Bunda na Mkono wanafunzi waliopata ufaulu wa daraja la kwanza ni asilimia 91 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo na kuzipongeza shule hizo kwa kufanya vizuri.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Shule za Sekondari za Mkono (Butiama), Morembe Day (Manispaa ya Musoma), Busegwe, Chiefu Ihunyo na Kiagata (Butiama) na Nyamunga (Rorya) wanafunzi wake wamepata ufaulu wa daraja la kwanza na la pili pekee.
Aidha, Bwana Bulenga amesema asilimia 45 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo walichaguliwa kuanza kidato cha tano wakiwa na ufaulu wa daraja la tatu na wengi wao sasa wamepata daraja la kwanza na la pili.
Bwana Bulenga amesema Mkoa umepata ufaulu wa asilimia 100 huku Mkoa wa Mara ukiwa na wastani wa GPA 2.059 na kati ya shule 29 zilizoshiriki mtihani huo, shule 23 zikiwa ni za Serikali na shule sita za binafsi.
Tukio hilo lilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu, baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na wajumbe wa Kamati ya Wataalamu waliokagua miradi ya mbio za Mwenge katika Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa