Mkuu wa Mkoa wa Mara leo amepokea makombe ya ushindi ya mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo Shule za Sekondari Tanzania (UMISETA) kitaifa na kutaka Mkoa kuboresha maandalizi ya ushiriki katika mashindano hayo ili kufanya vizuri zaidi.
Akizungumza mara baada ya kupokea vikombe hivyo, Mhe. Mtambi amezipongeza timu za Mkoa kwa kufanya vizuri katika mashindano hayo na kuutaka Mkoa kuboresha zaidi maandalizi ya wananfunzi wanaoshiriki michezo ili kupata timu bora zaidi.
“Katika historia ya michezo hapa nchini, Mkoa wa Mara umekuwa ukitoa wachezaji wazuri sana, tujipange vizuri na tuboreshe maandalizi yetu tunaweza kufanya vizuri zaidi” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, Mhe. Mtambi ameitaka Sehemu ya Elimu kuwaendeleza wanafunzi wenye vipaji katika michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na vyama vya michezo hiyo ili kuendeleza vipaji vya wanafunzi hao.
Akitoa taarifa ya mashindano hayo, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Mwalimu Makwasa Bulenga amesema Mkoa wa Mara umefanikiwa kupata jumla ya makombe sita na medali 50 ambapo makombe matano na medali 31 yametokana na UMITASHUMTA na kombe moja na medali 19 limetokana na UMISETA.
Bwana Bulenga amesema katika mashindano ya UMITASHUMTA Mkoa umeshika nafasi ya 2 Kitaifa kati ya mikoa 31 iliyoshiriki katika mashindano ya UMITASHUMTA na nafasi ya 17 kitaifa kati ya mikoa 28 iliyoshiriki katika mashindano ya UMISETA.
“Michezo tuliyofanya vizuri ni riadha wanawake, riadha wanaume, soka wanawake, handball wanawake na usafi na nidhamu wanaume katika UMITASHUMTA na katika UMISETA Mara iliongoza katika riadha wanaume” amesema Mwalimu Bulenga.
Bwana Bulenga amesema ili kupata matokeo mazuri miaka inayokuja, Mkoa utaweka mkazo katika kuimarisha vitalu vya michezo ili kuwaandaa wachezaji wenye vipaji, kuongeza usimamizi wa wanamichezo katika Shule za Sekondari, kuongeza miundombinu na vifaa vya michezo katika shule zote za Mkoa wa Mara.
Mashindano ya 29 ya UMITASHUMTA na mashindano ya 45 UMISETA yalifanyika katika Manispaa ya Iringa na kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa tarehe 09 Juni, 2025 na kufungwa rasmi na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Said Omar Kipanga tarehe 18 Juni, 2025.
Mashindano ya 45 ya UMISETA yalifungwa rasmi tarehe 29 Juni, 2025 na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Festo Dugange yakiwa na kauli mbiu isemayo “viongozi bora ni msingi wa Maendeleo ya Taaluma, Sanaa na Michezo, Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu”.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amepokea taarifa ya Kamati ya Wataalamu iliyoundwa kufuatilia miradi ya Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Mara na kuipongeza kamati hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuahidi kuyafanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyobainika katika maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025.
Aidha, amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa Ndugu Gerald Musabila Kusaya kufuatilia miradi iliyopangwa kutembelewa na Mwenge ambayo ilibainika kuwa na changamoto mbalimbali katika Halmashauri za Mkoa wa Mara ili iweze kufanyiwa kazi na kufuatiliwa ukamilishaji wake.
Mkoa wa Mara unatarajiwa kupokea Mwenge wa Uhuru tarehe 15 Agosti, 2025 kutoka Mkoa wa Simiyu ambapo utakimbizwa katika Halmashauri zote tisa kabla ya kukabidhiwa Mkoa wa Mwanza kuendelea na mbio zake.
Tukio hilo lilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu, baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na wajumbe wa Kamati ya Wataalamu waliokagua miradi ya mbio za Mwenge katika Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa