Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amewaapisha wakuu wa Wilaya za Butiama na Serengeti walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Juni, 2025 na kuwataka wakuu wa Wilaya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Akizungumza katika hafla ya kuwaapisha Angelina Marco Lubela Mkuu wa Wilaya ya Serengeti na Thecla George Mkuchika Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe. Mtambi amesema malalamiko, Kero na migogoro ya wananchi ikitatuliwa kwa wakati itasaidia kuleta amani na utulivu katika jamii na kuwarahisishia wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo.
“Migogoro na kero za wananchi ikitatuliwa kwa wakati, itawasaidia wananchi kutumia muda wao kufanya shughuli za maendeleo na kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya kusimamia mchakato wa uchaguzi katika maeneo yao ili mchakato mzima ufanyike kwa ukweli, uwazi na kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kuwaonya wote watakaoharibu kwa namna yoyote shughuli za uchaguzi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kanali Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara kusimamia suala la utoaji wa chakula shuleni na kuwahamasisha wazazi, walezi, wadau na wananchi kwa ujumla kuchangia chakula shuleni ili wanafunzi wapate angalau mlo mmoja shuleni.
Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya kuzisimamia Halmashauri katika ukusanyaji wa mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuimarisha makusayo ya Halmashauri na kuzifanya ziwe imara kiuchumi kuwahudumia wananchi kwa huduma mbalimbali.
Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao na kusimamia kuzigeuza changamoto mbalimbali watakazokutana nazo kuwa fursa za kimaendeleo.
Mhe. Mtambi amewapongeza Wakuu wa Wilaya hao kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Mhe. Rais na kuwataka kwenda kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali katika Wilaya zao.
Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka amewapongeza Wakuu wa Wilaya hao kwa kuteuliwa na Mhe. Rais kuziongoza Wilaya na kuwaahidi kuwa Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara watawapa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Mkoa wa Mara tunaishi kwa mshikamano na kushirikiana kama familia moja katika kuwahudumia na kutatua kero za wananchi na kutekeleza maagizo ya viongozi wetu” amesema Mhe. Chikoka.
Mhe. Chikoka amemshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kuwaamini kuziongoza Wilaya zao na kuwahakikishia Wakuu wa Wilaya wapya watapata ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Uapisho wa Wakuu wa Wilaya umehudhuriwa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Ndugu Iddi Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya nyingine za Mkoa wa Mara.
Wengine waliohudhuria ni Kamati ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Mara, Menejimenti na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara pamoja na ndugu, jamaa na marafiki za wakuu wa Wilaya walioapishwa.
Hafla ya uapisho inafuatia uteuzi wa viongozi hao uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutangazwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu tarehe 23 Juni, 2025.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa