Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara leo tarehe 05 Machi, 2025 ameongoza hafla ya kukabidhi magari matatu yaliyotolewa na Shirika llisilo la kiserikali la Amref kwa ajili ya kusaidia shughuli za usimamizi wa sekta ya afya katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi magari hayo, Bwana kusaya amewataka maafisa wanaokabidhiwa magari hayo kuyatumia vizuri kwenye shughuli za usimamizi wa sekta ya afya zilizokusudiwa na Shirika la Amref.
“Mimi nitafuatilia kwa karibu matumizi ya magari haya ili yatumike kwa makusudio yaliyopangwa ikiwa ni pamoja na kufuatilia muda wa matengenezo” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amelishukuru Shirika la Amref kwa kutoa msaada wa magari hayo na ni nyenzo muhimu katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Mara na kuahidi kuwa magari haya tutayatunza ili yaendelee kutoa huduma.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya Dkt. Zabroni Masatu amesema kuwa magari yaliyopokelewa ni Nissan Patrol moja kwa ajili ya matumizi ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na magari mawili Toyota hardtop ambayo yamekabidhiwa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Dkt. Masatu amelishukuru Shirika la Amref kwa msaada huo na kusema kuwa mahitaji ya magari ya usimamizi wa shughuli mbalimbali ya sekta za afya ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa miradi ya sekta hiyo na vituo vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Mkoa wa Mara Dkt. Revocatus Masanja amesema Amref imetoa magari matatu yaliyokuwa yanatumika kwa ajili ya usimamizi wa mradi wa ukimwi katika Mkoa wa Mara kwa ajili ya Halmashauri na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kutokana na shirika hilo kuona mahitaji.
“Magari haya bado ni mazima yakitumika vizuri yatasaidia kutatua uhaba wa changamoto za magari kwa ajili ya usimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya na miradi ya sekta ya afya” amesema Dkt. Masanja.
Dkt. Masanja ameishukuru Serikali ya Mkoa wa Mara kwa ushirikiano mkubwa ambao umekuwa ukitoa kwa wadau mbalimbali ikiwemo Shirika la Amref na kuupongeza Mkoa kwa kujali afya za wananchi wake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Bwana Msongera Palera amelishukuru Shirika la Amref kwa kutoa msaada huo ambao utatatua upunguvu mkubwa wa magari katika Halmashauri hiyo.
“Awali tulikuwa tunaazima magari Amref mara kwa mara na sasa wameona watupatie gari moja iwe ya kwetu ili tuweze kuwahudumia wananchi vizuri zaidi” amesema Bwana Palera.
Bwana Palera amesema Halmashauri yao ina eneo kubwa sana na inavituo vingi vya kutolea huduma za afya kwenye vimesambaa maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo na inakuwa vigumu kwa wasimamizi wa sekta ya afya kama hawana usafiri wa uhakika.
Hafla ya mapokezi ya magari hayo imehudhuriwa na baadhi ya watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Divisheni za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Halmashauri hizo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa