Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Masoko wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bwana Mrisho Mrisho amesema Mkoa wa Mara una fursa nyingi kwa kazi za Sanaa kutokana na kuwepo kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na migodi mikubwa ya madini.
“Mkoa wa Mara kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii, tozo na makusanyo mengine unatakiwa kuona namna ya kutumia fedha hizo kuibua na kukuza vipaji vya sanaa kwa vijana wadogo tangu ngazi ya shule” amesema Bwana Mrisho.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Biashara kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara Bwana Mrisho amesema faida kubwa ya mifumo ya Serikali kusomana kuwa ni pamoja na kuongeza ufanisi wa kazi na kuondoa usumbufu kwa wasanii na wadau wengine.
Bwana Mrisho amesema awali mifumo ilikuwa haisomani na kusababisha wadau ikiwemo wasanii kudanganywa na kupewa vibali feki jambo ambalo amesema kwa sasa halipo tena baada ya Serikali kurekebisha tatizo hilo.
Ndugu Mrisho amesema taasisi ikishasajiliwa na BASATA inapata faida nyingi kwa kuwa BASATA ina aina zote za wataalamu kutoka idara kadhaa ikiwamo ya sheria, mipango na TEHAMA wanaomsaidia mteja kwa kumpa ushauri wa bure wa kitaalamu na kumwezesha kufanyakazi kwa uhuru.
Kwa upande wake Afisa Utamaduni Mkoa wa Mara mwalimu Makondo Makondo ameishukuru BASATA kwa kuwawezesha wataalamu wa Mkoa wa Mara kupata mafunzo hayo ili kuweza kuwasaidia wasanii mbalimbali waliopo katika Mkoa.
Bwana Makondo amesema kuwa kwa maazimio haya waliyokubaliana katika mafunzo haya sasa Mkoa wa Mara unaweza kuwa na matamasha makubwa ya Kitaifa katika ngazi za Shule za Msingi na Sekondari.
Bwana Makondo amesema shule zina vilabu vya masuala mbalimbali ikiwemo kupinga rushwa, mazingira na michezo ambavyo vinafanya vizuri sana mashuleni na kupendekeza kuanzishwa klabu mahususi ya masuala ya Sanaa ili wanafunzi waweze kujifunza wakiwa wadogo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa